Korona: Sekta mbalimbali zinavyobadili sera za kiutendaji kulinda wafanyakazi na kupunguza maambukizi

0
39

Mlipuko wa homa ya kirusi cha corona umelazimisha sekta nyingi kutazama upya namna zinavyoendesha kazi zake. Katika juhudi za kupunguza maambukizi na kulinda wafanyakazi sekta nyingi zimejaribu kutengeneza sera mpya kiutendaji. 

Nchini Tanzania, Mamlaka ya Usafiri wa Anga mwanzoni ilichukua hatua ya kuzuia ndege zote za Kimataifa huku uamuzi pia ukifanyika kufunga shule kwa muda, kusitisha shughuli za kimichezo na mikusanyiko mikubwa ya umma mpaka pale hali itakapoonekana walau imetengemaa. 

Katika hatua nyingine upo uwezekano wa kampuni katika sekta mbalimbali kuendelea kupunguza mikutano ya uso kwa uso, makongamano, safari za nje na badala yake kutumia zaidi mtandao kuendesha mawasiliano na mikutano ya kibiashara. 

Mabadiliko haya japo yanasaidia biashara na shughuli kuendelea kama kawaida yanaleta pia changamato katika mipango mingi ambayo inahitaji zaidi ya mawasiliano ya kidijitali ili kufanikiwa. Mifano ni mingi, mfano mmojawapo ni takwa la kisheria la kampuni mbalimbali kuorodhesha hisa zao katika soko la hisa. Mchakato wake huhitaji mikutano mingi ya uso kwa uso, uhakiki na uwasilishaji mambo ambayo wakati kama huu yana changamoto kubwa kufanyika na hivyo kuzifanya kampuni mfano Tigo Tanzania ambazo zilitakiwa kuwa katika soko la hisa la Dar es Salaam kusogeza mbele muda wa kutekeleza agizo hilo. 

Utafiti unaonyesha kwamba katika nyakati hizi, kadiri tunavyopunguza na kusogeza mbele yale yanayoweza kusubiri, ndivyo tunavyopata muda na rasilimali za kuelekeza kwenye kuondoa changamoto ya gonjwa hili linalotukabili. 

Send this to a friend