Kubenea apewa siku 14 kuwaomba radhi Kikwete na Kinana

0
51

Rais Mstaafu, Dkt. Jakaya Kikwete na Makamu Mwenyekiti wa CCM, Abdulrahman Kinana wametoa siku 14 kwa gazeti la MwanaHalisi na mhariri wake, Saed Kubenea kuomba radhi pamoja na kufuta kashfa iliyochapishwa na gazeti hilo ikidai viongozi hao wanawafadhili wanaopinga mkataba wa Dubai na Bandari.

Viongozi hao pia wamemtaka Kubenea kutoa kiapo cha kisheria, kwamba yeye na gazeti analolihariri wanaahidi kuacha kuwakashifu, kutoa namna yoyote ya lugha isiyofaa, maneno ya uongo, kero au uchafuzi dhidi yao, na endapo wakishindwa hatua za kisheria zitachukuliwa.

Kwa mujibu wa barua ya Wakili Eric S. Ng’maryo iliyokwenda kwa Kubenea na kampuni ya Hali Halisi Publishers imesema Gazeti la MwanaHalisi toleo la Julai 20 hadi 26, mwaka huu limechapisha taarifa kuwa Kikwete na Kinana wamekuwa wakiwalipa watu fedha ili waendelee kupinga uwekezaji wa bandari jambo ambalo linawadhalilisha viongozi hao.

Prof. Assad: Wengi wanaozungumzia bandari si wataalamu wa uwekezaji

“Kashfa inayozungumziwa ni habari ya mbele inayosomeka ‘Sakata la Bandari’ huku ikiwahusisha wateja wetu pamoja na kuwekwa kwa picha zao. [..] Habari hiyo inawadhalilisha wateja [Dkt. Kikwete na Kinana] kwa kutamkwa moja kwa moja,” imesema taarifa.

Taarifa hiyo imeongeza kuwa tamko la kufuta kashfa na kuwaomba radhi viongozi hao linatakiwa kutojumlisha udhuru, stahili au mashaka na kwamba kabla ya kuchapishwa, tamko hilo liwasilishwe kwa kampuni hiyo ya mawakili kwa ajili ya kuhakikiwa.

Send this to a friend