Kulala chini ya saa 7 huchochea magonjwa ya moyo

0
5

Kulala ni moja ya mahitaji muhimu ya mwili, sawa na chakula na maji. Watu wengi wanadharau usingizi kwa sababu ya ratiba ngumu au kazi nyingi bila kujua madhara yake kwa afya ya akili na mwili.

Tafiti zinaonyesha kuwa kulala chini ya saa 6 hadi7 kwa siku mara kwa mara kunaweza kusababisha matatizo haya yafuatayo;

Madhara kwa Afya ya Akili

Kupungua kwa kumbukumbu na uwezo wa Kujifunza
Kulala husaidia ubongo kuchakata na kuhifadhi taarifa mpya. Ukikosa usingizi wa kutosha, uwezo wa kujifunza mambo mapya na kukumbuka hupungua.

Kuongezeka kwa mfadhaiko na msongo wa mawazo
Ukosefu wa usingizi huongeza kiwango cha homoni ya stress (cortisol), ambayo inaweza kusababisha msongo wa mawazo, huzuni, na hata kuongezeka kwa wasiwasi.

Kupungua kwa uwezo wa kufikiri na kufanya maamuzi
Uchovu wa ubongo huathiri uwezo wa mtu kufanya maamuzi sahihi, kuzingatia mambo muhimu, na hata kutatua matatizo kwa ufanisi.

Kuongezeka kwa hatari ya magonjwa ya akili
Ukosefu wa usingizi wa kutosha kwa muda mrefu umehusishwa na ongezeko la magonjwa kama vile wasiwasi, mfadhaiko, na hata hatari ya kupata matatizo ya akili kama schizophrenia.

Madhara kwa Afya ya Mwili
Kuongeza hatari ya magonjwa ya moyo
Tafiti zinaonyesha kuwa ukilala saa chache kwa muda mrefu, una hatari kubwa ya kupata shinikizo la damu, ugonjwa wa moyo, na kiharusi.

Kuongeza uzito na hatari ya kisukari
Ukosefu wa usingizi huathiri homoni zinazosimamia hamu ya kula, na kusababisha mtu kula zaidi. Hii huongeza hatari ya unene kupita kiasi na ugonjwa wa kisukari aina ya pili.

Kudhoofisha kinga ya mwili
Usingizi wa kutosha huimarisha mfumo wa kinga. Ukilala kidogo, mwili wako unakuwa dhaifu kupambana na maambukizi na magonjwa.