Kupanda na kushuka kwa Dkt. Bashiru Ally, kutoka uhadhiri, katibu mkuu hadi ubunge

0
29

Kwa siku chache zilizopita jina la Balozi Dkt. Bashiru Ally Kakurwa limegonga vichwa vya habari kutokana na kauli yake aliyoitoa juu ya uhusiano unaotakiwa kuwepo kati ya wakulima wadogo na Serikali.

Leo hatutajikita kwenye hoja hiyo, lakini zaidi kummulika na kumjua kwa ufupi Bashiru Ally ni nani, amepita wapi, hadi kufika hapo alipo sasa.

Balozi Dkt. Bashiru Ally Kakurwa alizaliwa mkoani Kagera Januari 1, 1968.

Alisoma Shule ya Msingi Katerero kati ya mwaka 1980 na 1986 kabla ya kujiunga na Sekondari ya Kilosa mwaka 1987 hadi 1990.

Kisha akajiunga na Shule ya Sekondari ya Ihungo kwa elimu ya juu kati ya 1991 na 1993 kabla ya kuendelea na masomo ya shahada tatu katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).

Balozi Dkt. Bashiru Ally Kakurwa ana Shahada ya Sayansi ya Siasa na Utawala wa Umma (BA in Political Science and Public Administration), Shahada ya Uzamili (MA) na Shahada ya Uzamivu (PhD), zote kutoka UDSM.

Alianza Utumishi wa Umma katika Chuo Kikuu cha Mzumbe, Morogoro kama Mhadhiri Msaidizi kuanzia Septemba, 2003 hadi Septemba, 2004. Aidha, Balozi Bashiru ametumia taaluma yake kama Mhadhiri (Lecturer) katika Idara ya Sayansi ya Siasa na Utawala wa Umma ya CKD kuanzia Oktoba, 2004 hadi Mei, 2018.

Vilevile, amekuwa Kiongozi wa Umoja wa Wahadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDASA) kwa nafasi ya Makamu Mwenyekiti na Mwenyekiti kati ya mwaka 2014 na mwaka 2016. Balozi Dkt. Bashiru pia alikuwa Mkurugenzi wa Kurugenzi ya Utandawazi, Mikutano/Mihadhara na Uendelezaji (Director of Internationalisation, Convocation and Advancement) katika CKD.

Balozi Bashiru ni mwanafunzi wa falsafa ya Mwalimu Julius Kambarage Nyerere (Baba wa Taifa) kuhusu harakati za ukombozi, sera za kutofungamana na upande wowote, Umoja wa Afrika, ujamaa na kujitegemea.

Aliteuliwa na Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Hayati Dkt. John Pombe Joseph Magufuli kuwa Katibu Mkuu wa CCM kuanzia Juni, 2018 hadi Februari, 2021. Uteuzi huo ulitokana na kazi aliyoifanya akiwa Kiongozi wa Timu iliyofuatilia na kurejesha mali za CCM mwaka 2017/2018.

Tarehe 26 Februari, 2021 Dkt. Magufuli alimteua Dkt. Bashiru Ally Kakurwa kuwa Balozi na Katibu Mkuu Kiongozi.

Katika nafasi ya Katibu Mkuu Kiongozi, Dkt. Balozi Bashiru ni Katibu Mkuu wa Rais, Katibu wa Baraza la Mawaziri (BLM), Mkuu wa Utumishi wa Umma na Katibu wa Baraza la Usalama la Taifa (BUT).

Aliitumikia nafasi hiyo kwa muda mfupi hadi Machi 31, 2021, kufuatia Rais Samia Suluhu Hassan kumteua Balozi Hussein Kattanga kuwa Katibu Mkuu Kiongozi wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Machi 31, 2021 aliteuliwa na Rais Samia kuwa Mbunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, nafasi ambayo anaendelea kuitumikia.

Send this to a friend