Kutoka kufuata shule 30km, hadi 2km. Tanga wamshukuru Rais Samia

0
36

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Muheza, Nassibu Mmbaga amesema bila uwepo wa mradi wa fedha za ustawi wa Taifa wa mapambano dhidi ya UVIKO-19 ingewachukua miaka mingi kujenga vyumba vya madarasa 67, yakiwemo ya shule shikizi 10.

Mmbaga ameyasema hayo wilayani Muheza mkoani Tanga wakati akielezea mafanikio yaliyotokana na fedha hizo katika kutatua changamoto kwenye halmashauri yake.

Halmashauri hiyo ilipatiwa TZS bilioni 1.4 kwa ajili ya ujenzi wa madarasa hayo ambapo kwa bajeti ya halmashauri ingechukua miaka 21 kuweza kujenga madarasa hayo.

Amesema mbali na kwamba madarasa hasa ya shule shikizi yatatoa mazingira mazuri kwa ajili ya wananfunzi kujisomea, lakini pia yatapunguza umbali ambao wanafunzi hao walikuwa wakitembea kila siku kufuata shule.

“Uwepo wa shule shikizi utasaidia kuwapunguzia umbali wa mwendo wanaotembelea watoto hasa wanaoanza shule ya awali hadi darasa la tatu. Watoto wamepata ahueni, pamoja na muda mzuri wa kukaa na kusoma kwa ufanisi. Walikuwa wanatembea umbali wa kilomita zaidi ya 10, lakini sasa wanatembea kilomita moja hadi mbili,” amesema Mmbaga.

Amemshukuru Rais kwani kupitia fedha hizo wameweza kupata madarasa mengi kuliko waliyokuwa wanahitaji.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Mji wa Handeni, Maryam Ukwaju amesema walipokea TZS milioni 740, na zilitumika katika utekelezaji wa ujenzi vyumba vya madarasa 37, kati hivyo 22 vya sekondari 15 kwa ajili ya shule shikizi.

“Maeneo yote yaliyojengwa vyumba vya madarasa yalikuwa na uhitaji mkubwa kwa sababu watoto ni wengi. Baadhi yao walikuwa wanatembea muda mrefu hasa wanaoishi kata ya Bondo ambao walikuwa wanatembea hadi kilomita 30 kwenda na kurudi kufuata shule kuu ya Kwalua,” amesema.

 

 

Send this to a friend