Taifa la Iran kwa sasa liko katika simanzi kufuatia kifo cha Rais wao, Ebrahim Raisi ambaye amefariki katika ajali ya helikopta iliyokuwa imembeba yeye pamoja na Waziri wa Mambo ya Nje wa nchi hiyo na wengine saba na kuanguka eneo la milimani karibu na Azerbaijan kutokana na hali mbaya ya hewa.
Hata hivyo, kumekuwa na na mijadala mingi inayoendelea kuwa huenda Israel ambaye ni adui mkuu wa Iran amehusika na ajali hiyo kutokana na mambo yanayoendelea baina yao, huku hoja nyingine zikiibuliwa kuhusu uwezekano wa maadui wa ndani kuhusika kutokana na utawala wa Raisi ‘uliojaa utata.’
“Nahisi ilikuwa ni mauaji. Tutaona kama Iran itachunguza kwa kina. Nahisi Israel iko nyuma ya hili,” mtumiaji mmoja wa mitandao ya kijamii alisema Jumatatu.
Israel inahusishwa kutokana na kuongezeka kwa mvutano wa hivi karibuni kati yao ikiwa ni pamoja na mauaji ya Jenerali wa Iran huko Damascus, Mohammad Reza Zahedi, na mashambulizi makubwa ya ndege zisizo na rubani na makombora yaliyofanywa na Iran mwezi uliopita.
Kwa upande wa Israel ilizindua shambulio lake dhidi ya mfumo wa rada ya ulinzi wa anga katika mji wa Isfahan, Iran bila kusababisha vifo lakini ikitoa ujumbe wa wazi.
Kwanini kuna ugomvi baina yao?
Israel imekuwa ikiiona Iran kama tishio kubwa kwa sababu ya mpango wake wa nyuklia wenye utata, makombora yake ya masafa marefu na msaada wake kwa vikundi vya silaha vinavyoapa kuangamiza Israel, huku Iran ikijiona kama mdhamini mkuu wa wapinzani wa Israel (Palestina) dhidi ya utawala wa Israeli, wakitaka Israel ifutwe kutoka kwenye ramani.
Raisi, ambaye alikuwa na msimamo mkali aliikemea Israel mwezi uliopita akisema “utawala wa Kizayuni wa Israeli umekuwa ukikandamiza watu wa Palestina kwa miaka 75.”
“Kwanza kabisa tunapaswa kuwafukuza wavamizi, pili tunapaswa kuwafanya walipe gharama za uharibifu wote waliouleta, na tatu, tunapaswa kuwafikisha mbele ya haki mnyanyasaji na mvamizi,” alisema.
Malanga alivyokuwa nyuma ya jaribio la mapinduzi DRC na jinsi Marekani inavyohusishwa
Katika taarifa iliyotolewa hivi karibuni na kituo cha habari cha Reuters kutoka kwa Afisa mmoja wa Israel ambaye hakutaka jina lake litambuliwe, amekanusha madai hayo akisema kuwa “hatukuwa sisi”.
Hata hivyo, mpaka sasa hakuna ushahidi wa moja kwa moja kuwa Israel ilihusika na ajali ya helikopta siku ya Jumapili.