Kwanini Mkoa wa Kagera ni mkoa masikini zaidi nchini?

0
69

Mkoa wa Kagera unapatikana Kaskazini-Magharibi mwa Tanzania. Jina lake linatokana na mto Kagera.

Mkoa huu unapakana na nchi ya Uganda kwa Kaskazini, Rwanda na Burundi kwa upande wa Magharibi.

Katika sekta ya uchumi, mwaka 1994 Kagera ilishika nafasi ya 12 kati ya mikoa 21 kwa hali ya uchumi nchini. Mwaka 2022 ikashika nafasi ya 26 kati ya mikoa 26, ikimaanisha kwamba ndio Mkoa Masikini zaidi nchini.

Asilimia 51 ya wakazi wake wanatumia chini ya TZS 1,644 kwa siku (mstari wa umasikini Tanzania ni TZS 49,320 kwa Mwezi ) huku pato la wastani la mtu wa Kagera ni TZS milioni 1.2 kwa mwaka. Mtu wa Ruvuma na Iringa ana pato la wastani mara 3 zaidi ya mtu wa Kagera.

Mkoa wa Kagera ni Mkoa wenye ardhi iliyopandwa kahawa kuliko Mkoa wowote nchini, una utajiri mkubwa wa ardhi na hali ya hewa nzuri, pia ni mkoa uliokaa kimkakati, kijiografia (unapakana na nchi nyingi zaidi za Afrika Mashariki kuliko mikoa mingine), wenye rasilimali madini kama Nickel na wasomi wengi zaidi kuliko mikoa mingi ya Tanzania.

Swali ni Je! Kwanini Mkoa huu unatajwa kuwa Mkoa masikini zaidi nchini Tanzania licha ya kuwa na rasilimali hizo zilizotajwa?

Hizi ni sababu kadhaa;

1. Uchumi wa Kagera unategemea sana kilimo ambacho kinategemea mvua, hivyo, ukame au mvua zinazopungua zinaweza kusababisha upungufu wa chakula na mapato kwa wakazi wa mkoa huo. Hii pia inasababishwa na sera zilizopitwa na wakati kuhusu masoko ya mazao ya kilimo na haswa kahawa kiasi cha wakazi wa Kagera kupeleka kahawa Uganda.

2. Miundombinu ya barabara na reli katika Mkoa huo ni duni na kufanya usafirishaji wa mazao na bidhaa kuwa mgumu na gharama kuwa kubwa.

Licha ya kuwa Mkoa huu uliathiriwa sana na vita vya Kagera, hapakuwa na mpango maalumu wa kuhuisha uchumi wa Kagera baada ya vita na ndio maana kumekuwa na mdororo wa uchumi wa Mkoa huu.

3. Elimu na afya ni changamoto kubwa katika Mkoa wa Kagera. Huduma za afya na elimu zinapatikana kwa kiwango kidogo, hivyo kusababisha wakazi wa Mkoa huo kuwa na ugumu wa kupata huduma hizo.

4. Kagera ilipata athari kubwa ya tetemeko la ardhi mwaka 2016 ambapo nyumba nyingi na miundombinu iliharibiwa na kusababisha hasara kubwa kwa wananchi pamoja na uchumi wa mkoa huo.

Send this to a friend