LATRA: Haturidhishwi na huduma zitolewazo na Mwendokasi

0
22

Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri Ardhini (LATRA) imesema hairidhishwi na huduma za mabasi yaendayo haraka (UDART) na ndiyo sababu ongezeko la nauli mpya halijahusisha usafiri wa mwendokasi.

Ameyasema hayo Mkurugenzi Mkuu wa LATRA, Habibu Suluo wakati wa mahojiano na Clouds FM ambapo amesema tangu mwaka 2022 LATRA iliwapa masharti ya kuboresha huduma ikiwa ni pamoja na kuhakikisha upatikanaji wa huduma hiyo.

“Sasa hivi huduma zake haturidhiki nazo na tumeshawaandikia. Na mnakumbuka katika hizi nauli hatujapandisha nauli za Mwendokasi, nauli zake tulizitangaza tarehe 30, Desemba mwaka 2022,” ameeleza.

Ameongeza kuwa “Ukiona mpaka leo kuna zile daladala tangu tumeanza [mwaka 2016] maana yake ni kuwa tumeona mahitaji hayajatosha, na mwezi mmoja uliopita tumetangaza kuongeza mabasi katika njia hiyo ya Kimara baada ya kuona watu wanarundikana pale [vituo vya mwendokasi].”

Hata hivyo amesema LATRA haina mamlaka ya moja kwa moja na Mwendokasi kwa sababu iko chini ya Wizara ya TAMISEMI, hivyo LATRA inaangalia ubora na kutoa leseni lakini haiwezi kusimamisha kutoa huduma.

“Unajua ile DART iko chini ya TAMISEMI sisi tuko Wizara ya Uchukuzi. [..] hatuwezi kuwa na mamlaka ya moja kwa moja na mwendokasi  kwa sababu tuko chini ya wizara nyingine, sisi tunaangalia usawa wa ubora, tunawapa leseni lakini hatuwezi kumsimamisha kwamba hakuna tena hii huduma lazima tufanye consultation [mashauriano],” ameeleza.

Send this to a friend