Mkurugenzi wa Mamlaka Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA), Johansen Kaatano amesema mamlaka inajiandaa kuwasajili na kuwapa vyeti makondakta wa daladala na mabasi yaendayo mikoani ili kuboresha huduma kwa watumiaji.
Kaatano amesema kumekuwa na malalamiko kutoka kwa abiria kuhusu huduma zitolewazo na makondakta hasa wa daladala kutokana na wengi kutokuwa na elimu ya uelewa na udhibiti mdogo.
“Atakayepewa kazi ya ukondakta aingie darasani na asome, akishasoma apewe cheti, asajiliwe halafu ndipo awe na sifa ya kufanya hivyo. Kwa hiyo mwenye basi hataenda kuokota mtu huko mtaani, lazima aingie kwenye mfumo wa mamlaka.”
Aidha amesema, itakuwa kosa la mwenye basi kama atamuajiri kondakta ambaye hajasajiliwa na mamlaka husika.
Ameongeza kuwa, kama kutakuwa na kondakta ambaye ni jeuri na anasumbua abiria mamlaka ikipokea taarifa zake mara kadhaa, kondakta huyo ataondolewa kwenye mfumo.