LATRA: Tutawafungia madereva wa Uber na Bolt wanaofanya udanganyifu wa nauli  

0
42

Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) imewataka watumiaji wa huduma ya usafiri wa mtandaoni kutoa taarifa haraka kwenye mamlaka hiyo wanapofanyiwa udanganyifu wa nauli kutoka kwa madereva.

Akizungumza na Swahili Times Mkurugenzi wa Udhibiti Usafiri wa Barabarani, Johansen Kahatano amesema hawajapata malalamiko rasmi kutoka kwa wateja, hivyo abiria anapokutana na hali yoyote ya tofauti atoe taarifa akiambanisha namba ya gari au pikipiki pamoja na namba ya simu ya dereva ili kufanya uchunguzi.

“Huduma hiyo ni mpya hivyo sheria haijabainisha sana kwenye suala la udanganyifu, lakini kama wakibainika, sisi tuna mamlaka ya kuwafuta kwenye huduma hiyo moja kwa moja,” amesema.

Ameongeza, ”inabidi tukae tuiangalie vizuri tujue kama ni kweli kuna matendo ya jinsi hiyo yanatokea, tuna haja ya kuangalia upya sheria zetu ili kujua ni hatua zipi tunaweza kuchukua kuwadhibiti hao wanaofanya udanganyifu kwenye mfumo wetu,” amesisitiza Kahatano.

Ndege tatu za ATCL zasimamishwa kuendelea na kazi

Aidha, amesema viwango vya nauli vilivyopangwa na LATRA kwa kilometa moja ni kati ya TZS 800 hadi TZS 1,000 huku kwa dakika ni TZS 80 hadi 100 hivyo  watumiaji wakilinganisha muda na umbali wanaweza kujua ni kiasi gani ambacho kimetumika, na kujua kama kuna udanganyifu umefanyika.

Kwa upande wa malalamiko yanayohusisha ukubwa wa makato kwa madereva kuwa chanzo cha udanganyifu, Kahatano amebainisha kuwa jambo hilo halihalalishi kuchukua hatua ya kuwarubuni wateja, badala yake wanapaswa kutoa malalamiko yao kwa mamlaka na wao watawasikiliza.

Send this to a friend