LATRA yatangaza bei mpya ya nauli

0
53

Mamlaka ya Udhibiti wa usafiri Ardhini (LATRA) imetangaza ongezeko la nauli za mabasi ya mwendokasi jijini Dar es Salaam zitakazoanza kutumika siku 14 zijazo kuanzia leo Jumanne Januari 03, 2023.

Mkurugenzi Mkuu wa Latra, Habibu Suluo amesema nauli hizo zimeongezeka kwa TZS 100 kutoka nauli za zamani na kutangaza nauli mpya elekezi kwa teksi mtandao, pamoja na viwango vipya ambavyo viko katika makundi manne ambayo ni magari ya kubeba abiria sita, abiria wanne, pikipiki ya magurudumu matatu (bajaji) na ile ya magurudumu mawili.

Suluo amesema nauli ya mabasi ya mwendokasi kwa njia kuu (truck route) ni TZS 750 kutoka TZS 650, njia ya mlisho (feeder router) ni TZS 500 kutoka TZS 400, njia ya mlisho na njia kuu (feeder +truck route) ni TZS 900 kutoka TZS 800 na njia ya kimara kwenda Kibaha ni TZS 700 badala ya pendekezo la DART la TZS 1,200.

Kwa upande wa nauli za teksi mtandao zinazobeba abiria wanne nauli itakuwa TZS 3,000 hadi 4,000 kwa safari isiyozidi kilomita moja, na kama kuna safari nyingine kutoka hapo nauli itaongezeka kwa TZS 800 hadi 1,000 kwa kilomita moja, endapo safari itakutana na vikwazo kama foleni nauli ya ziada itaongezeka kwa TZS 80 hadi TZS 100 kwa dakika.

Kwa upande wa magari yanayobeba abiria sita, nauli elekezi ni TZS 4,000 hadi TZS 5,000 kwa safari isiyozidi kilomita moja, na kama kutakuwa na safari ya ziada toka ya awali nauli itaongezeka kwa TZS 1,000 hadi TZS 1,200 kwa kilomita moja, endapo vitatokea vikwazo kama foleni nauli, itaongezeka kwa TZS 80 hadi TZS 150 kwa dakika.

Kwa nauli za pikipiki ya kubeba abiria wawili, nauli elekezi itakuwa TZS 1,000 hadi TZS 1,500 kwa safari isiyozidi kilomita moja, na kama safari itaongezeka kutoka hapo nauli itaongezeka kwa TZS 300 hadi TZS 400 kwa kilomita moja, na endapo kutakuwa na vikwazo kama foleni nauli itaongezeka kwa TZS 50 hadi TZS 70 kwa dakika.

“Kwa upande wa nauli za pikipiki mtandao zinazobeba abiria wasiozidi watatu ni nauli TZS 2,000 hadi TZS 2,500 kwa safari isiyozidi kilomita moja na safari ya ziada itakayongezeka nauli itaongezeka kwa TZS 500 hadi TZS 600 kwa kilomita moja, na kama kutakuwa na vikwazo njiani kama foleni nauli itaongezeka kwa TZS 70 hadi TZS 90 kwa dakika moja,” amesema Suluo.

Suluo amesema bado wapo kwenye vikao vya masikilizano na wadau kuhusu nauli za treni ya mwendokasi (SGR) na tayari wamepokea mapendekezo kutoka kwa Serikali na bei kamili ya nauli hizo itatangazwa mwezi ujao baada ya kuwasili kwa mabehewa nchini.

“Mapendekezo haya ni kwa mujibu wa sheria lakini kama kuna mdau yeyote ana malalamiko au hakubaliani na haya alete malalamiko yake ndani ya siku 14 kutoka leo,” amesema.

Hata hivyo, Latra imelikataa ombi la kuongeza nauli kwa wanafunzi na kubakia TZS 200 iliyokuwepo.

Chanzo: Mwananchi

Send this to a friend