Ligi Kuu ya NBC kurejea mwanzoni mwa mwezi Februari

0
36

Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) imetangaza kurejea kwa michezo ya Ligi Kuu ya NBC katika juma la kwanza la Februari, 2025 ambayo awali ilipangwa kuendelea Machi 1, 2025 baada ya kutamatika kwa michuano ya Kombe la Mapinduzi na fainali za Mataifa ya Afrika kwa Wachezaji wa Ndani (CHAN).

TPLB imesema michezo hiyo itarejea kwa michezo ya viporo kabla ya kuendelea na michezo ya mzunguko wa 17, ambapo tarehe rasmi pamoja na ratiba iliyofanyiwa maboresho zitatangazwa hivi karibuni.

Aidha, Bodi ya Ligi imetoa wito kwa klabu zote kuhakikisha zinaongeza nguvu katika maandalizi ya timu zao kiufundi pamoja na masuala mengine hasa yahusuyo miundombinu ya viwanja ambavyo vitakaguliwa kabla ya kurejea kwa ligi.

Mabadiliko hayo yamekuja baada ya Shirikisho la Soka Afrika (CAF) kusogeza mbele fainali za CHAN kutoka Februari 1, 2025 hadi Agosti, 2025, hivyo kutoa nafasi kwa Bodi ya Ligi Kuu Tanzania kuendelea na michezo ya Ligi Kuu ya NBC ambayo ilisimama kupisha fainali hizo.

Send this to a friend