LINDI: Askari amuua kwa risasi dereva lori akijihami

0
53

Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Lindi amesema kuwa dereva aliyekuwa anaendesha gari la Dangote aliuawa kwa kupigwa risasi na askari polisi wakati akijaribu kumpora askari huyo silaha.

Taarifa ya Kamanda Mtatiro Kitinkwi imeeleza kuwa dereva huyo alimchoma kwa visu askari huyo akitaka kuiba silaha yake, ndipo askari akafanikiwa kumdhibiti baada ya kumjeruhi kwa risasi na kupelekea kifo chake.

Kabla ya tukio hilo lililotokea Oktoba 17 mwaka huu majira ya saa 5 usiku, eneo la Jamhuri mkoani Lindi Kitinkwi amesema askari wanne walisimamisha gari hilo aina ya lori lililokuwa likiendeshwa na Ibrahimu Said (miaka 30-35) akiwa na mwwenzake.

Kamanda huyo amesema dereva huyo alikaidi amri ya kusimama na kumgonga askari aliyekuwa akimsimamisha, ndipo gari hilo likaacha njia na kugonga mti.

Baada ya hapo dereva huyo alishuka na kwenda kumvamia askari mwingine aliyekuwa na silaha na kuanza kumchoma visu sehemu mbalimbali za mwili wake akiwa na lengo la kupora silaha.

Katika tukio hilo afisa mmoja na askari wawili wamejeruhiwa katika mapambano hayo, na wamelazwa katika Hospitali ya Sokoine na afya zao zinaendelea vizuri.

Hata hivyo jeshi hilo halijaeleza mtu mwingine aliyekuwa kwenye lori hilo ni nani, na yuko wapi.

Jeshi hilo limewataka wananchi kutii sheria bila shuruti.

Send this to a friend