Maabara ya Taifa ya Jamii kupima ubora wa majibu kwa magonjwa ya binadamu

0
17

Serikali kupitia Maabara ya Taifa ya Afya ya Jamii imeanza kuandaa sampuli kwa ajili ya kupima ubora wa majibu yanayopimwa kwa magonjwa ili kuweza kutoa huduma za matibabu sahihi kupitia watoa huduma za afya nchini.

Ameyasema hayo jijini Dar es Salaam kaimu mkurugenzi wa maabara hiyo, Medard Beyanga wakati akiongea na Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Wizara ya Afya, Catherine Sungura alipotembelea maabara hiyo.

Beyanga amesema maabara hiyo yenye viwango vya kimataifa, imeanza kutengeneza sampuli za upimaji ubora wa huduma za maabara na kuzipeleka katika maabara za mikoa, ambapo maabara zilizopo mikoani hupima sampuli hizo na majibu yake hurudishwa maabara ya Taifa na kupima ubora wa majibu yaliyopimwa.

“Tunataka kuhakikisha mgonjwa anayepimwa kote nchini anakuwa na majibu sahihi, mgonjwa akipimwa kipimo mkoa mmoja akienda kupimwa mkoa mwingine majibu yafanane ili kuwasaidia watoa huduma katika kutoa huduma bora za matibabu,” amesema Beyanga.

Hata hivyo ameishukuru Serikali kwa kuwapatia mashine na vifaa vya kisasa vyenye uwezo wa kupima magonjwa tofauti tofauti na kwamba hakutakuwa haja ya kupeleka sampuli nje ya nchi kama ilivyokuwa hapo awali.

Rais Samia alivyodokeza mwisho wa bosi wa TPA

Kwa upande wa upimaji wa UVIKO-19 amesema hivi sasa wamekuwa na mafanikio makubwa na kuweza kuwarahisishia wananchi pamoja na wasafiri huduma za upimaji wa ugonjwa huo kwa kuwa wameongeza vituo kwenye baadhi ya maeneo nchini.

Send this to a friend