Maagizo 9 ya Makamu wa Rais ufunguzi wa Nane Nane

0
40

Makamu wa Rais, Philip Mpango amefungua rasmi maonesho ya sherehe za wakulima, wafugaji na wavuvi ‘Nane Nane’ katika viwanja vya John Mwakangale jijini Mbeya.

Katika hotuba yake, haya ni maagizo tisa aliyoyatoa  Makamu wa Rais;

1) “Ninazitaka halmashauri zote zitenge bajeti kwenye mipango yao ili kusaidia maafisa mifugo kwenda kutoa huduma za ugani kwa wafugaji.”

2) ”Ninaitaka Ofisi ya Waziri Mkuu kuweka mfumo ambao utawezesha wizara za kisekta kusimamia na kufuatilia utendaji wa wataalamu wa Sekta zao ambao wako kwenye halmashauri.”

3) ”Napenda kuwaagiza taasisi zetu za utafiti kujiongeza na kutafiti mbegu ambazo zinazaa zaidi, lakini pia mazao mapya ambayo yanastawi vizuri katika kila mkoa.”

4) “Kutokana na upungufu wa malighafi  na vifungashio ambavyo vinauzwa kwa bei kubwa, baadhi havina ubora na pia havipatikani kwa urahisi. Ninapenda kuwakumbusha tena Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara pamoja na sekta binafsi kushughulikia  jambo hili.

Napenda kutoa maelekezo yafuatayo, lumbesa sasa hapana. Mazao kama viazi, vitunguu, mpunga sasa yauzwe kwa kupimwa  kwenye mizani, na hili lifanyike katika Mikoa yote.

5) “Nasisitiza na kuelekeza vyuo na taasisi zetu za umma kama DIT, SIDO n.k  na taasisi binafsi kubuni teknolojia rafiki za kuhifadhi na kusindika mazao ya biashara ili tuepuke uharibifu wa mazao yasiyoweza kuhifadhiwa kwa muda mrefu.”

6) “Ninaziagiza wizara za kisekta zinazohusika zishirikiane na Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara pamoja na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kutafuta na kupanua wigo wa masoko ya bidhaa zetu.”

7) “Ninazihimiza kaya zote, tusiuze kila kitu, tujiwekee akiba ya chakula. Na kwa upande wa wafugaji wachukue fursa hii kupunguza mifugo yao na wahifadhi fedha ziwasaidie katika ununuzi wa chakula huko mbele.”

Nataka niwakumbushe Wizara ya Kilimo, Wakala wa Taifa wa hifadhi ya Chakula, NFRA na bodi ya mazao mchanganyiko mwendelee kufuatilia kwa ukaribu na kufanya tathmini ya hali ya chakula katika nchi yetu ili tuhakikishe nchi inabaki kuwa na akiba ya kutosha ya chakula.”

8) “Ninapenda kutoa rai kwa taasisi za fedha kuendeleza  jitihada za kuweka masharti nafuu ya upatikanaji wa mikopo kwa wakulima, wafugaji na wavuvi, na kuzitangaza ili kuongeza uwekezaji na uzalishaji katika sekta hizo na kupunguza changamoto za ajira.”

9) “Nataka niiagize Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara mshirikiane na Wizara ya Fedha na Mipango kupitia TRA na Bodi ya biashara ya nje muweze kubaini ukubwa na kiini cha wafanyabiashara wa Tanzania katika Mikoa ya mpakani , kuhamishia biashara zao upande wa baadhi ya nchi jirani katika ukanda huu.

Send this to a friend