Makamu wa Rais wa Tanzania, Dkt. Philip Mpango amekutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Tanzania nchini Indonesia, Macocha Tembele ambapo amemuagiza kuendelea kuitangaza lugha ya Kiswahili katika nchi hiyo ikiwemo kutafuta namna ya lugha hiyo kufundishwa nchini Indonesia.
Katika mazungumzo hayo yaliofanyika Jijini Dar es Salaam, Dkt. Mpango amemuagiza Tembele kuhakikisha anakuwa na nyenzo muhimu zinazobeba vipaumbele vya nchi kama vile dira ya maendeleo ya taifa, mpango wa maendeleo wa miaka mitano pamoja na ilani ya Chama Cha Mapinduzi ya 2020.
Pia amemuagiza kuhakikisha anashiriki katika mikutano mbalimbali itakayowezesha kueleza mazuri ya Tanzania, kuvutia wawekezaji pamoja na kuwaunganisha Watanzania wanaoishi Indonesia ili waweze kuchangia maendeleo ya Tanzania.
Mbali na hayo amemtaka Tembele kuhakikisha anatekeleza diplomasia ya uchumi kwa kutafuta masoko ya bidhaa zinazozalishwa Tanzania, na kutafuta teknolojia rafiki zitakazoweza kusaidia katika kuongeza thamani ya bidhaa zinazozalishwa Tanzania.