Maamuzi yaliyofikiwa katika mkutano wa Wakuu wa Nchi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki

0
14

Wakuu wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) wamepokea taarifa ya uhakiki na kuagiza Baraza la Mawaziri la EAC kuharakisha mchakato wa majadiliano ya Mkataba (accession treaty) yatakayowezesha DR Congo kuwa mwanachama, na kuwasilisha taarifa hiyo katika mkutano wa kawaida utakaofanyika mapema mwaka 2022.

Viongozi hao wametoa agizo hilo wakati wa Mkutano Maalum wa 18 uliofanyika leo kwa njia ya mtandao, ambapo suala la DR Congo lilikuwa ni moja ya ajenda mbili za mkutano huo.

Ajenda ya pili ilihusu pendekezo la mabadiliko ya kanuni ya 11(1) inayohusu akidi ya mikutano ya wakuu wa nchi na wanachama wa jumuiya hiyo ambapo wameagiza Baraza la Mawaziri la kisekta la Sheria na Mahakama kukutana kujadili pendekezo la mabadiliko ya Kanuni ya 11 (1) ya uendeshaji wa Mikutano ya Wakuu wa Nchi Wanachama na kuwasilisha ripoti hiyo katika Mkutano ujao wa kawaida kwa lengo la kujadili na kukamilisha suala hilo.

Aidha, Wakuu wa Nchi na Serikali wa Jumuiya ya Afrika Mashariki wamemkaribisha na kumpongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa utendaji wake tangu ashike wadhifa huo.

Akihutubia kwa mara ya kwanza katika Mkutano huo, Rais Samia amewashukuru viongozi wa jumuiya hiyo kwa ushirikiano mkubwa na kuahidi kuwa Tanzania itashiriki kikamilifu katika kuhakikisha kuwa jumuiya inatimiza malengo yake.

Send this to a friend