
Rais Samia Suluhu Hassan ameendelea kusimamia maboresho makubwa katika Sekta ya Uchukuzi, hususan katika Bandari ya Tanga, ambayo sasa ina uwezo wa kuhudumia meli kubwa moja kwa moja kutoka nje ya nchi.
Hayo yamesemwa leo Machi Mosi, 2025 na Waziri wa Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa na kubainisha kuwa, serikali imewekeza kiasi cha shilingi bilioni 419.16 katika maboresho ya Bandari ya Tanga, jambo ambalo limeleta matokeo makubwa, ikiwemo ongezeko la shehena kutoka tani 750,000 hadi tani 3,000,000 kwa mwaka.
“Pia, idadi ya meli zinazoingia bandarini imeongezeka kutoka meli 118 mwaka 2019/2020 hadi kufikia meli 307 mwaka 2023/2024.” amesema Profesa Mbarawa.
Katika hatua nyingine, maboresho hayo yamesababisha kupungua kwa muda wa kuhudumiwa kwa meli kutoka siku tano hadi siku mbili, jambo lililopunguza gharama za uendeshaji na kuongeza ushindani wa bandari hiyo katika ukanda wa Afrika Mashariki.
Zaidi ya hayo, mapato ya Bandari ya Tanga yameongezeka kwa kasi kubwa, ambapo ndani ya miezi saba tu ya mwaka wa fedha 2024/2025, Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) imekusanya shilingi bilioni 49.84.
Maboresho haya pia yamechangia kwa kiasi kikubwa katika ongezeko la ajira, ambapo kabla ya maboresho, bandari ilikuwa ikiajiri wastani wa wafanyakazi wa muda mfupi 6,630 kwa mwezi, lakini sasa imefikia wastani wa 17,871 kwa mwezi.
Ameongeza kuwa, Serikali imeendelea kusimamia maendeleo zaidi katika sekta ya uchukuzi mkoani Tanga, ambapo miradi mbalimbali yenye thamani ya shilingi trilioni 1.1 inatarajiwa kutekelezwa katika mwaka wa fedha 2025/2026.
Miradi hiyo inahusisha ukarabati wa reli inayoingia bandarini yenye urefu wa kilometa 3.9 pamoja na kituo cha reli ndani ya Bandari ya Tanga, mradi unaotarajiwa kugharimu shilingi milioni 980.