Serikali inakusudia kutoa majengo matatu ya Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) yaliyopo Mtaa wa Nyamwezi na Mkunguni karibu na Soko Kuu la Kariakoo jijini Dar es Salaam, yafanyiwe maboresho kwa ajili ya kutumiwa na wafanyabiashara wadogo (Machinga).
Uamuzi huo umefuatia wafanyabiashara hao kuandika barua Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) kuomba kupatiwa sehemu za kufanyia biashara kwenye majengo ya NHC yaliyopo Kariakoo kufuatia Seriali kuamua kuwaondoa wale waliokuwa wakifanya biashara maeneo ya barabarani.
“TAMISEMI walianisha mitaa ya Tandamiti na Msimbazi kwa ajili ya wafanyabiashara wadogo lakini maeneo hayo yameonesha kutokidhi mahitaji lakini sisi tumeona majengo matatu yaliyopo mtaa wa Nyamwezi na Mkunguni,’’ amesema Naibu Waziri Dkt Mabula, Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akiwa ziarani kwenye eneo hilo.
Mabula ameitaka NHC kulichukulia suala hilo kwa umuhimu mkubwa na haraka kutokana na changamoto zake na kusisitiza kuwa wakati hatua za utekelezaji maendelezo ya majengo yaliyoainishwa ukifanyika ni vyema kila kitu kikawekwa ili wafanyabiashara wakaelewa muelekeo wao.
Makamu Mwenyekiti wa Shirikisho la Wamachinga Tanzania, Stephen Lusinde kwa upande wake alisifu uamuzi w Dkt. Mabula kutembelea majengo ya NHC yaliyoainishwa na kubainisha kuwa hatua hiyo inaonesha kuwa sasa mambo yanaweza kukaa vizuri kwa wamachinga kupata muelekeo wa wapi pa kwenda.