Madagascar: Waziri afukuzwa baada ya kuagiza pipi za bilioni 5
Waziri wa Elimu nchini Madagascar amefukuzwa kazi baada ya mpango wake wa kutaka kununua pipi zenye thamani ya $2.2 milioni (TZS 5.1 bilioni) kugundulika.
Rijasoa Andriamanana aliagiza pipi hizo wiki iliyopita kwa ajili ya watoto kumumunya ili kuondoa uchungu wa wa dawa ya corona inayotumiwa nchini humo (Covid-Organic).
Dawa hiyo imetengenezwa kutokana na mimea ya asili kwa ajili ya kukabiliana na Covid-19, hata hivyo Shirika la Afya Duniani (WHO) halijaipitisha kuwa inatibu ugonjwa huo.
Shirika la Habari la Ufaransa (AFP) limesema kuwa kila mwanafunzi nchini humo alikuwa apewe pipi tatu.