Miezi miwili tangu ilipolengeza masharti ya kukabiliana na maambukizi ya virusi vya corona ikiwa ni pamoja na kufungua shule, Mji Mkuu wa Madagascar, Antananarivo umerejesha tena masharti ikiwa ni pamoja na wananchi kutakiwa kukaa ndani (lockdown).
Amri ya wananchi kubaki majumbani inatarajiwa kutekelezwa kwa wiki mbili hadi Julai 20, ambapo mtu mmoja tu katika kila familia ndiye ataruhusiwa kutoka nje kati ya saa 12 asubuhi hadi saa 6 mchana.
Mamlaka ya afya nchini humo imeripoti kuongezeka kwa visa vya corona ambapo Julai 4 mwaka huu ilirekodi jumla ya visa 216, kiwango kikubwa zaidi kuwahi kurekodiwa kwa siku moja.
Hadi sasa nchi hiyo imeripoti jumla ya visa 2,941, ambapo kati ya hivyo watu 1,014 wamepona huku 32 wakifariki dunia.
Taifa hilo limekuwa likisambaza dawa ya asili katika baadhi ya nchi za Afrika kwa maelezo kuwa inawasaidia watu wenye maambukizi ya virusi hivyo, lakini bado haijathibitishwa na mamlaka za afya za kimataifa.