Madaktari feki wakamatwa Muhimbili

0
50

Hospitali ya Taifa Muhimbili imewakamata madaktari feki wawili waliojitambulisha kwa jina la Josephat Joseph na Khamis Hamad Bakari baada ya uongozi wa hospitali hiyo kupata taarifa kutoka kwa raia wema.

Watuhumiwa hao wamedaiwa kuwahadaa wagonjwa na ndugu zao kuwa wao ni madaktari na kutumia mwanya huo kujipatia fedha isivyo halali, ambapo uongozi uliweka mtego baada ya kupata taarifa hizo na kufanikiwa kuwakamata.

Josephat Joseph amekamatwa katika kliniki ya magonjwa ya Ngozi Februari 27, mwaka huu huku Hamis Hamad Bakari ambaye alikuwa akishirikiana naye alikamatwa maeneo ya Taasisi ya Tiba ya Mifupa Muhimbili (MOI).

Watuhumiwa hao wamefikishwa katika Kituo Kikuu cha Kati kilichopo jijini Dar es Salaam kwa ajili ya hatua za kisheria.

Aidha, hospitali imetoa rai kwa wananchi kuchukua tahadhari ikiwemo kutoa taarifa kwa uongozi wa hospitalli pale wanapomtilia shaka mtoa huduma ili kuepuka watu wenye nia ovu kama hao na kuwaelekeza watumishi wa hospitali hiyo kuvaa vitambulisho muda wote wa kazi ili jamii iweze kuwatambua kwa urahisi.

“Pia tunawakumbusha wananchi kwamba malipo yote ya hospitali yanafanyika kupitia kumbukumbu namba (control number) ambapo ukilipia huduma, jina la Hospitali ya Taifa Muhimbili litatokea,” imeeleza taarifa kutoka uongozi wa Muhimbilli.

Send this to a friend