Madaktari waeleza madhara ya kutumia mate kama kilainishi wakati wa kujamiiana

0
72

Wataalam wa afya wamewatahadharisha watu wanaotumia mate ukeni kama kilainishi kwa ajili ya kuleta ladha wakati wa kujamiiana kwamba kunaongeza magonjwa yanayosababishwa na maambukizi ya fangasi na bakteria katika via vya uzazi vya mwanamke, ambayo husababisha kutokwa uchafu na harufu mbaya ukeni.

Wataalam wamedai kuwa, magonjwa hayo ambayo huonesha dalili mbalimbali yasipotibiwa kwa wakati husababisha bakteria na virusi hao kushambulia zaidi uke na kupanda taratibu mpaka katika via vya uzazi vya mwanamke, hivyo kusababisha ugonjwa wa maambukizi katika via vya uzazi (PID).

Daktari bingwa wa magonjwa ya mfumo wa uzazi na wanawake kutoka Hospitali ya Agha Khan, Jane Muzo amesema unapochukua mate na kuyaweka katika uke unahamisha bakteria wanaopatikana katika mdomo na kuwaleta katika uke, hivyo bakteria hao wanapokuwa wakali husababisha saratani ya kizazi, uvimbe na magonjwa mengine ya mfumo wa uzazi.

Aidha, Daktari bingwa wa magonjwa ya uzazi na wanawake kutoka Hosipitali ya Salaaman, Temeke, Abdu Mkeyenge amebainisha kuwa mwanaume anaweza kuwa na maambukizi ya fangasi au bakteria na wengine kwenye kinywa, hivyo anavyoyatoa mate husababisha maambukizi ikiwa ni pamoja na kupata vipele.

Amesema wapo wanawake wanaopata madhara makubwa zaidi ikiwemo kutokwa na maji machachu wakati wa tendo la ndoa na hivyo kupoteza thamani yao hali ambayo isipopatiwa ufumbuzi kwa wakati tatizo huwa kubwa zaidi ikiwemo kupata ugumba, ujauzito kutunga nje ya uzazi, kuwa na mkusanyiko wa usaha katika sehemu za nyonga na madhara mengine.

Dk. Mkenyenge ameshauri wanaume kuwaandaa vizuri wenza wao wakati wa kufanya tendo la ndoa badala ya kutumia mate.

“Ukimwandaa vizuri kuna majimaji ambayo anaweza kuyatoa ndiyo yanayosaidia kulainisha sehemu za siri, hata baadaye ukija kumwagilia hatahisi maumivu yoyote wala karaha. Wanaume wengi hawawaandai ipasavyo, hivyo baadae wanapata michubuko na wanaumia, hapo ndipo mwanaume anatafuta suluhisho la haraka wanatumia mate,” amesema.

Chanzo: Mwananchi

Send this to a friend