Madalali Dar walalamikia Wachina kuingilia kazi za udalali

Dar es Salaam, Tanzania - 25 June 2023: Cityscape of masaki, an administrative ward in Kinondoni District of the Dar es Salaam Region in Tanzania.
Madalali wanaofanya shughuli zao katika maeneo ya Masaki na Oysterbay, Dar es Salaam, wameiomba Serikali iingilie kati kutokana na kuingiliwa kwa biashara yao na raia wa kigeni, hasa Wachina, wanaodaiwa kufanya biashara ya udalali wanapoingia nchini.
Akizungumza na Swahili Times, Kaimu Katibu wa Madalali katika maeneo hayo, Ally Kasi, ameeleza kuwa raia hao wa kigeni husaidiwa na baadhi ya Watanzania wakiwemo madereva na wakalimani, jambo linalorahisisha shughuli zao zisizo rasmi katika soko la upangishaji wa nyumba.
“Anaweza akaja kwangu akanambia anahitaji nimwoneshe nyumba zinazopangishwa, namzungusha, na anaweza akakwambia hii nyumba mbaya hatuitaki, kumbe jioni karudi pale kampa mlinzi elfu 10 au 20, inategemeana na mtu aliyemkuta. Anachukua namba ya mwenye nyumba halafu anaongea na mwenye nyumba,” amesema.
Ameongeza kuwa baadhi yao huongeza bei ya upangishaji kwa makusudi ili kupata kamisheni ya siri. “Kwa mfano, nyumba ni dola 5,000 [TZS milioni 13] kwa mwezi, yeye anamwambia mwenye nyumba ‘nakuja na mchina mwenzangu, mwambie ni dola 5,500 [TZS milioni 14.2], hiyo 500 [TZS milioni 1.3] kila mwezi itakuwa yangu mwaka huu, mwakani utachukua wewe.'”
Kasi amesema tayari wameshawasilisha malalamiko hayo kwa baadhi ya viongozi wa Serikali, akiwemo Waziri wa Viwanda na Biashara, Dkt. Selemani Jafo, na wameahidiwa kuwa suala hilo linafanyiwa kazi.







