Madhara ya kuvaa miwani ya urembo

0
88

Uvaaji miwani ya jua (Sunglasses) ni aina ya mtindo wa muda mrefu unaotumika kuongeza mvuto katika vazi, mbali na hilo husaidia kukinga macho dhidi ya miale ya jua. Watu wengi hususani vijana wa kisasa wanavutiwa zaidi na miwani ya jua pasipo kufahamu kuwa kuna madhara yanayoweza kujitokeza endapo miwani itavaliwa pasipo kupimwa.

Wataalam wanasema kuvaa miwani ya jua ndani ya nyumba haitadhuru kuona kwako, lakini inaweza kuchosha macho yako, na kusababisha uchovu wa macho. Hii inaweza kusababisha maumivu ya kichwa na kutoona vizuri.

Mara nyingi hutokea zaidi hasa kwa miwani ya jua yenye ubora duni wa lenzi, hii inaweza kuongeza mkazo wa macho yako.

Daktari bingwa wa upasuaji wa macho, Neema Daniel Kanyaro amewahi kuzungumza katika kituo cha redio hapa nchini na kusema, watu wengi wamekuwa wakivaa miwani pasipo kujua kwamba zinaweza kuwasababishia matatizo ya kuona.

Dkt. Kanyaro alifafanua kwamba, watu wamekuwa wakivaa miwani za jua kama urembo pasipo kwenda kupima na kujua ni aina gani ya miwani wanazotakiwa kuzitumia lakini pia bila kujua kama miwani hizo zina namba kwakuwa kila mtu ana namba kutokana na uono wake.

Alishauri kuwa “Miwani ni dawa lakini usivae bila kupima kwani inaweza kukusababishia matatizo ikiwemo uoni hafifu. Unaweza kukuta unavaa miwani nyeusi lakini kumbe siyo namba yako. Kama hujijui unaweza kuta ukitazama unaona giza kumbe umeshaua macho kwa urembo.”