Maeneo 12 ambayo hutakiwi ku-overtake gari jingine

0
49

1) DARAJANI: Epuka kupita gari jingine kwenye daraja, kwani linakubana unakuwa huna sehemu nyingine ya kuchepukia zaidi ya kutumbukia mtoni endapo gari jingine litakuwa mbele yako. Hii inaweza kupelekea kugongana uso kwa uso na gari linalokuja mbele.

2) KONA: Kwenye kona, usithubutu kupita gari jingine, haijalishi unaona upenyo kiasi gani. Ni hatari kwani huwezi kujua kama kuna gari linakuja ama la.

3) MLIMAN: Kama ilivyo kwenye kona, milima na vilima ni sehemu mbaya kupita gari jingine kwani huoni mbele vizuri, na utapata changamoto kuendesha gari kwa kasi sana kupita lingine ili kuepuka kugonga na yanayotokea upande mwingine.

4) MITEREMKO MIKALI: Hatari hapa inatokana na uwezekano wa breki za gari kushindwa kufanya kazi kwa ufanisi.

5) KAMA HUONI MBELE VIZURI: Kwa sababu yoyote. ile, kama huoni mbele vizuri epuka kishawishi cha kupita gari jingine.

6) MVUA: Mvua ikiwa kubwa sana, epuka kupita magari barabarani kwani barabara huteleza na pengine unaweza usiwe unaona mbele vizuri.

7) MSAFARA: Misafara huwa inakwenda kwa kasi sana, na magari huachiana nafasi ndogo. Hatari ya kujaribu kupita msafara kwanza magari hayo huwa kasi, pili unaweza kukosa nafasi ya kujichomeka gari linapotokeza mbele yako.

8) BARABARA NYEMBAMBA: Endapo barabara ni nyembamba na haiwezi kumudu magari mawili yanayokwenda sambamba, kaa utulie.

9) UTELEZI: Mvua, maji maji, aina ya udongo, hivi vinaweza kufanya barabara kuwa na utelezi, chukua tahadhari sana unapotaka kupita gari katika maeneo yenye utelezi.

10) MADEREVA WAKOROFI: Kuna madereva ambao huona barabara kama sehemu ya mashindano. Hawa huongeza mwendo kila unapotaka kumpita. Unapoona unakabiliana na dereva wa aina hiyo, epuka kumpita kwani anaweza kukusababishia madhara.

Huna haja ya kumthibitishia kwamba wewe ni bora zaidi yake. Mashindano yenu yanaweza kuwafikisha kaburini.

11) GARI PINZANI: Kama gari linalokuja upande mwingine hulioni vizuri, au huwezi kukadiria umbali ambao gari hilo lipo na mwendo wake, usijaribu kupita gari la mbele yako kwa kudhani kwamba dereva wa gari linalokuja mbele yako anakuona.

12) USIKU: Kuendesha gari usiku kunahitaji tahadhari na umakini sana. Kama huoni vizuri, usipite gari jingine. Lakini muhimu kama una matatizo ya macho, changamoto za kuona vizuri usiku, usiendeshe gari usiku. Kama ikikubidi, endesha kwa tahadhari sana.

Usalama wako na wa watumiaji wengine wa barabara unaanza na wewe. Zingatia sheria za usalama barabarani upuke ajali zinazoweza kusababisha vifo au ulemavu.

Send this to a friend