Maeneo 7 ya ushirikiano yaliyoridhiwa kati ya Tanzania na Zambia

0
47

Rais Samia Suluhu Hassan amefanya mazungumzo na Rais wa Zambia, Hakainde Hichilema aliyewasili nchini leo kwa ajili ya ziara ya kikazi inayolenga kukuza ushirikiano na biashara baina ya mataifa hayo mawili.

Katika hotuba yake, Rais Samia Suluhu ameeleza makubaliano yalifanyika baina ya Tanzania na Zambia;

• Uhusiano wa kisiasa
“Nchi zetu kwa yoyote yale yaliyotokea lakini ni lazima turudi, sisi kama viongozi wa nchi tuwaongoze watu wetu waelewane vizuri.”

• Usalama wa nchi
“Tumeangalia kwenye ukanda huu mambo yanayotokea, ugaidi na mambo mengine kadhaa, tukasema turudi tuwe na ushirikiano mkubwa kwenye mambo ya usalama wa nchi zetu.”

• Hali ya kiuchumi
“Tumekubaliana kwamba kwa dunia ya leo reli ni SGR, kwa hiyo tumekubaliana kuwa na mradi wa pamoja, tutafute fedha pamoja kupitia PPP kushirikiana na sekta binafsi pengine na wenzetu marafiki waliotujengea hiyo reli tuone jinsi tutakavyoiboresha kwenye kiwango cha SGR.”

• Biashara na Uwekezaji
“Tuna vikwazo vya kikodi na visivyo vya kikodi zinazofanya biashara zetu zisikue kama tulivyotarajia. Tumesema sekta za uwekezaji na biashara, lakini taasisi zetu za kukusanya mapato na taasisi zinazoshughulikia mambo ya customs tukae tuangalie nini ni kikwazo kwetu tuondoe ili biashara ziende vizuri.”

“Tumewazungumzia wafanyabiashara wadogo wadogo wanapovuka mipaka yetu kwenda kufanya biashara masharti wanayopewa ni makubwa. Kwanza permits [vibali] za kuingia, lakini tozo wanazotozwa ni kubwa mno.

• Tatizo la madereva
“Tumekubaliana taasisi za madereva, zile jumuiya zao Zambia na Tanzania tuziweke pamoja, wazungumze na Serikali zetu mbili tuangalie ni nini matakwa yao, tuwasikilize wanashida gani ili Serikali mbili zifanye kazi pamoja kuwatatulia shida zilizopo, ili madereva wetu wafanye kazi vizuri na tuondoe vile vikwazo pamoja mipakani vya kuchelewesha magari yanayopeleka biashara.”

• Sekta ya Nishati
“Mbali na Tazama Pipeline, kuna mradi mkubwa pia unaitwa Grid Interconnectivity ya Tanzania na Zambia. Huu ni mradi wa nchi tatu, Tanzania, Zambia na Kenya. Kila mmoja ameanza kufanya shughuli kule kwao, kwa upande wetu utekelezaji utaanza Januari mwakani.”

“Tutakwenda kuweka pool ya umeme mkubwa [..] ambapo kama nchi moja itapata tatizo nchi nyingine itasolve nchi jirani, au kama hatuna tatizo tutaweza kuuzia nchi ambazo hatuko nao pamoja. [..] ni green energy.”

• Mambo ya Kilimo (Soya)
“Tumekubaliana tusishindane lakini tuongezeane, tuongeze uzalishaji. Wenzetu ni mabingwa wameendelea kidogo wana mbengu nzuri, tumezungumza na nikawaambia kwamba linapokuja suala la mbegu mnatutoza pesa nyingi sana, akaniambia tuzungumze tuuziane kwa bei ya kirafiki na bei ya kindugu, Mawaziri wetu watakutana na watazungumza.”

“Tumekubaliana kufanya kazi kwa pamoja, na kama mmoja ana soko na kingine basi amwambie mwenzie soko liko hapa. Sisi leo tume offer [toa] soko la nyama, mbuzi na kondoo. Tuna soko kubwa tumelipata Saudi Arabia, Sisi peke yetu Tanzania hatuwezi kutimiza mahitaji yao, tumewaalika wenzetu waje tufanye mpango wa pamoja twende tukalitumie hilo soko.”

Send this to a friend