Magari 5 yenye gharama kubwa zadi duniani

0
91

Magari ya kifahari yamekuwa alama ya umahiri wa teknolojia na sanaa katika utengenezaji wa magari. Kila gari kati ya haya lina muundo wa kipekee, teknolojia ya hali ya juu, na uzuri wa ajabu unaowavutia wapenzi wa magari duniani kote.

Bei ya magari haya inafikia kiwango cha juu kutokana na ubora wa vifaa, nguvu ya injini, na umahiri wa kiufundi.

Hapa chini ni orodha ya baadhi ya magari ghali zaidi duniani;

1. Rolls-Royce La Rose Noire Droptail – TZS bilioni 81.9


Hili ni gari la viti viwili lenye paa linaloweza kuondolewa, tofauti na Rolls-Royce za awali za viti vinne. Bodi ya gari hili imetengenezwa kwa kaboni, chuma, na alumini. Lina urefu wa mita 5.3 na upana wa mita 2. Kitu cha kipekee ni rangi ya bodi yake, ambayo hubadilika unapoiangalia kutoka pembe tofauti. Rangi hii ilibuniwa baada ya majaribio 150 tofauti.

2. Rolls-Royce Boat Tail – TZS bilioni 76.4

Rolls-Royce imerejea kwenye biashara ya kutengeneza magari ya kipekee kupitia Boat Tail, yaliyotengenezwa kwa ufahari zaidi nje na ndani. Boat Tail pia ina “sehemu ya kuhudumia wageni” yenye friji ya champagne na mwavuli wa jua uliojengwa ndani. Tetesi zinaonyesha kuwa gari hili limegharimu dola milioni 28.

3. Bugatti La Voiture Noire – TZS bilioni 51

Bugatti La Voiture Noire (kwa Kifaransa ‘Gari Jeusi’) ina injini yenye nguvu ya quad-turbo 8-lita W16, bomba la moshi sita, na nembo ya nyuma inayong’aa. Gari hili linaunganisha kasi, uzuri, anasa, na teknolojia, likionyesha umahiri wa chapa ya Bugatti.

4. Pagani Zonda HP Barchetta – TZS bilioni 47.7

Kampuni ya Pagani, iliyoanzishwa na Horacio Pagani mwaka 1992, ni maarufu kwa magari yake ya kifahari. Zonda HP Barchetta ni gari la kipekee, moja kati ya magari matatu tu yaliyotengenezwa, huku moja likitengwa kwa ajili ya Pagani mwenyewe.

5. SP Automotive Chaos – TZS bilioni 39

Mbunifu wa magari kutoka Ugiriki, Spyros Panopoulos, ametengeneza magari yenye kasi ya ajabu. SP Automotive Chaos Earth Version ina nguvu ya farasi 2,048. Gari hili linaweza kufikia kasi ya 100 km/h kwa sekunde 1.55 na kukamilisha umbali wa robo maili kwa sekunde chini ya 7.5.