Mahakama Kuu mjini Mombasa imeamuru Serikali kuwapa wanaharakati wawili mikataba inayohusiana na ujenzi wa mradi wa reli ya kisasa (SGR) inayohusisha Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China na Serikali ya Kenya wenye thamani ya KSh bilioni 450 (TZS trilioni 9).
Wanaharakati Khelef Khalifa na Bi Wanjiru Gikonyo walitaka kandarasi, makubaliano na tafiti zote zinazohusiana na ujenzi na utendaji kazi wa SGR kuwekwa wazi. Walisema kuwa kuweka nyaraka hizo kwa usiri kunakiuka sheria na uwazi katika utawala.
Aidha, Jaji John Mativo amesema maafisa wa umma wana wajibu wa kikatiba kutoa habari kwa Wakenya akisema kwamba kizuizi chochote cha kupata habari kutoka kwa serikali lazima kiwe na madhumuni ya kweli na athari inayoonekana ya kulinda maslahi ya usalama wa taifa.
Kenya yafuta posho za vikao za wabunge
Walalamishi walisema kuwa hati zinazohusiana na mradi wa SGR na ufadhili wake hazijawahi kutangazwa kwa umma licha ya kuwa moja ya miradi ya gharama kubwa kufanywa na serikali.
“SGR ni mradi mkubwa zaidi wa miundombinu unaohitaji mtaji mkubwa kuwahi kujengwa nchini, lakini pamoja na matumizi haya ya ajabu ya fedha za umma, mradi huo umefanywa kwa utata na usiri tangu kuanzishwa kwake,” wamesema
Katibu Mkuu wa Uchukuzi, Joseph Njoroge alisema itakuwa ni ukiukaji wa masharti ya kimkataba ikiwa wanaharakati hao watapewa ufichuzi wa hati zinazohusiana na ujenzi wa mradi huo na kuongeza kuwa, iwapo maagizo yaliyoombwa yatakubaliwa, yataathiri uhusiano kati ya Kenya na China.
Hata hivyo Mwanasheria Mkuu, Kihara Kariuki alitaka ombi hilo kutupiliwa mbali na kusema Gikonyo na Khalifa hawakutumia njia zote za kutatua mizozo.