Mahakama Kenya yamhukumu kifo mwizi wa simu

0
6

Mahakama ya Kibera nchini Kenya imemhukumu Isaac Khanga adhabu mbili za kifo baada ya kupatikana na hatia katika makosa mawili ya unyang’anyi wa kutumia nguvu.

Khanga amehukumiwa kwa kuiba simu mbili za mkononi zenye thamani ya Ksh 39,000 [TZS 793,000] na pesa taslimu Ksh 30,000 [TZS 610,000] kwa kushirikiana na wenzake, huku wakitishia kuwadhuru wamiliki wa mali hizo usiku wa Novemba 3, 2024 katika eneo la Kawangware Madiaba, Kaunti Ndogo ya Dagoretti.

Katika tukio la kwanza, Khanga na wenzake walimvamia mtu na kuiba simu aina ya Tecno ya Ksh 24,000 pamoja na Ksh 30,000 taslimu. Katika tukio la pili, aliiba kwa nguvu simu nyingine ya Ksh 15,000.

Wakili Ann Murage, kutoka Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (ODPP), ameongoza kesi hiyo na kuthibitisha hatia ya Khanga pasi na shaka yoyote, na kumpa adhabu mbili za kifo kwa kila kosa licha ya wenzake kutoroka.

Hakimu Mkazi Christine Njagi amesema kuwa chini ya sheria za Kenya, adhabu ya kifo bado ni halali na haijabatilishwa na mahakama yoyote, akiongeza kuwa Khanga atatumikia adhabu moja ya kifo na nyingine itasimamishwa.