
Mahakama Kuu ya Kenya imetoa amri ya kuzuia utekelezaji wa mkataba wa ushirikiano wa afya kati ya Kenya na Marekani hususani kipengele kinachohusiana na uhamishaji wa taarifa za afya na taarifa binafsi, hadi uchunguzi ufanyike.
Kesi hiyo iliyowasilishwa na ‘Consumers Federation of Kenya’ (COFEK) imedai mkataba huo wa Ksh bilioni 200 [TZS Trilioni 3.81] unakiuka sheria na unaweza kusababisha taarifa za Wakenya kutumika vibaya nje ya nchi.
COFEK imesema mara tu taarifa za afya za Wakenya zitakapohamishwa nje ya nchi, madhara yake hayataweza kurekebishwa, na kwamba hakuna mahakama wala mamlaka yoyote ya Kenya itakayokuwa na uwezo wa kudhibiti jinsi taarifa hizo zitakavyotumiwa nje ya nchi, hali inayoweza kusababisha uvunjaji wa faragha, unyanyapaa, na matumizi mabaya ya taarifa.
Kesi hiyo itatajwa tena tarehe 12 Februari, 2026 mbele ya Jaji Lawrence Mugambi ili kuthibitisha kama amri imezingatiwa na kupanga tarehe ya kusikiliza haraka.
Jumatano, Rais William Ruto alikanusha madai kwamba Marekani iliishawishi Kenya kukubali mkataba huo. Akiongea Ikulu ya Nairobi kwenye mkutano wa 12 wa ushirikiano kati ya Serikali Kuu na Serikali za Kaunti, Ruto alisema kuwa serikali ya Kenya ndiyo iliyoanzisha mazungumzo, si Marekani kama inavyodaiwa.








