Mahakama ya Rufaa yabatilisha uamuzi wa Mahakama Kuu kesi ya dhamana za wahujumu uchumi

0
58

Mahakama ya Rufaa ya Tanzania imetengua uamuzi wa awali wa Mahakam Kuu na kusema kuwa makosa yaliyochini ya kifungu cha 148(5) cha Sheria ya Taratibu za Mwenendo wa Makosa ya Jinai yaendelee kuwa hayana dhamana.

Mahakama hiyo imetoa uamuzi huo leo ilipotupilia mbali uamuzi wa Mahakama Kuuu katika kesi iliyofunguliwa na Wakili Dickson Sanga Mei 9, 2019.

Wakili huyo alifungua kesi ya kikatiba kuhoji sheria inayonyima dhamana watu wenye tuhuma za mauaji, uhaini, ugaidi, wizi wa kutumia silaha na utakatishaji fedha ambapo alikuwa anaitaka Mahakama Kuu ya Tanzania kutangaza kipengele hicho cha sheria kuwa ni kinyume cha Katiba, huku akitaka kirekebishwe ili kutoa dhamana kwa watuhumiwa.

Mahakama Kuu ilimpa ushindi Wakili Sanga kwa kusema kuwa kifungu hicho kinakiuka katiba, na ndipo jopo la mawakili wa serikali walikata rufaa kupinga uamuzi huo.

Rufani hiyo ilisikilizwa mbele ya Jopo la Majaji Stella Mugasha, Gerald Ndika, Jacobs Mwambegele, Mwanaisha Kwariko na Ignas Kitusi ambapo upande wa warufani uliwakilishwa na Mawakili kutoka Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Dk Clement Mashamba, Biswalo Mganga, George Mandepo, Alesia Mbuya, Faraja Nchimbi, Abubakar Mrisha na Narindwa Sekimanga.

Upande wa mjibu rufani uliwakilishwa na mawakili Mpoki Mbuga, Jonathan na Jebra Kambole.

Katika rufaa hiyo warufani walisimama katika hoja mbalimbali ikiwemo, Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam kwamba ilifanya makosa ya
kisheria kushikilia kifungu namba 148(5) kwamba kinakiuka Ibara ya 13(3) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Kati ya sababu zilizomfanya Sanga kufungua kesi hiyo ni pamoja kudai kuwa uhuru binafsi na dhana ya kutokuwa na hatia ni haki ya kikatiba iliyohakikishwa katika ibara ya 13(6)(b) pamoja na ibara ya 15(1) na (2) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Pia alidai kifungu hicho kinachukua mamlaka ya mahakama ambayo ndiyo chombo chenye mamlaka ya kuamua haki za Watanzania ikiwa wana hatia au hawana kama ilivyoainishwa katika ibara ya 13(3).

Send this to a friend