Mahakama yaamuru nyumba iuzwe kulipia deni la mahari

0
58

Mahakama ya Wilaya ya Meatu imeamuru nyumba ya mkazi wa Kijiji cha Nkoma Mkoa wa Simiyu, Seleman Mussa (65), kuuzwa ili kulipa deni la mahari ya shilingi milioni 1.1 analodaiwa kijana wake.

Mussa amedai kijana wake ambaye ni mwalimu wa shule ya Sekondari mkoani Shinyanga alimuoa binti wa Mwita Kati (Justina) mwaka 2019 kwa ndoa ya kimila na kwa makubaliano ya mahari ya ng’ombe 15 wenye thamani ya shilingi 150,000 kila mmoja.

Amedai baada ya maridhiano hayo familia ya Justina ilidai mahari yote, lakini aliwaomba wachukue mahari nusu (TZS milioni 1.1) na nyingine watailipa baadaye. Ilipofika mwaka 2020, baba mzazi wa mwanamke huyo alianza kudai mahari iliyosalia na ndipo ugomvi ulipoanza hadi kufikishana mahakamani.

“Novemba 10, 2022 tulifika kwa Mkuu wa Wilaya Meatu, Fauzia Hamidu, huko niliahidi kupunguza na akatushauri turudi kwenye familia tukayamalize, nilipopata pesa nilienda kupunguza deni mbele ya Serikali ya kijiji kama mashahidi,” amesema.

Shauri la madai lilifunguliwa katika Mahakama ya Mwanzo, Meatu na hukumu ilitolewa chini ya Hakimu F. F. Madungu Mach 14, 2023 ikiamuru kukamatwa kwa nyumba ya Mussa iliyopo Kijiji cha Nkoma kufidia TZS milioni 1.1 ili kufikia TZS milioni 2.2 walizokubaliana.

TANAPA yatangaza gharama ya milioni 5 kwa anayetaka kumpa mnyama jina

Katika hati hiyo, mahakama imeeleza kuwa mdaiwa aliomba kuilipa pesa hiyo kidogo kidogo hadi Septemba, 2023, na mdai alikataa akitaka alipwe pesa yake kwa pamoja, ndipo aliiandikia barua mahakama akiomba kukamata nyumba ya mdaiwa.

Baada ya mdaiwa kusomewa barua ya maombi ya mdai, alisema deni litalipwa na mkwe wa mdai hivyo mdai aliomba aendelee na utekelezaji wa ombi kwa kuwa mdaiwa hataki kulipa.

Akizungumza na gazeti la Mwananchi mdai huyo, Mwita Kati amesema anataka pesa yake ilipwe kwa kuwa ni miaka mitatu sasa amekuwa akidai pesa hiyo bila mafanikio.

Chanzo: Mwananchi

Send this to a friend