Mahakama yaamuru nyumba ya mtoto wa Mbowe ipigwe mnada

0
53

Mahakama Kuu ya Tanzania imeamuru nyumba ya mkurugenzi wa gazeti la Tanzania Daima, Dudley Mbowe iliyoko eneo la Mikocheni Dar es Salaam ipigwe mnada ili kulipa deni la shilingi milioni 62.7 anazodaiwa na waliokuwa waandishi na wahariri wa gazeti hilo.

Mahakama imefikia uamuzi huo uliotolewa na Naibu Msajili wa Mahakama hiyo, Mary Mrio kufuatia maombi yaliyowasilishwa na waandishi hao, Maregesi Paul na wenzake tisa ili kutekeleza uamuzi wa Tume ya Usuluhishi na Uamuzi (CMA), katika shauri la mgogoro wa kikazi walilolifungua dhidi ya mwajiri huyo.

Aidha, mahakama hiyo pia imemteua Jesca Massawe, dalali kutoka kampuni ya udalali ya MM Auctioneer & Debt Collectors kutekeleza amri hiyo

Akizungumza na Mwananchi, Paul amesema wakati amri hiyo inatolewa, Dudley ambaye ni mtoto wa Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe hakuwepo mahakamani licha ya kuahidi kuwa angefika na fedha za kuwalipa.

Wanahabari hao walifungua shauri hilo la mgogoro wa kikazi baada ya mwajiri wao kuvunja mikataba ya ajira ambapo katika shauri hilo walikuwa wakiomba kulipwa jumla ya shilingi milioni 114. Hata hivyo katika uamuzi uliotolewa na CMA iliamuru wadai walipwe shilingi milioni 62.7 baada ya pande zote kufikia makubaliano.

Chanzo: Mwananchi