Aliyekuwa Mwenyekiti wa NCCR Mageuzi, James Mbatia ameshinda kesi dhidi ya Makamu Mwenyekiti wa chama hicho, Joseph Selasini ambaye alimfungulia mashtaka ya udhalilishaji dhidi yake.
Hukumu hiyo iliyotolewa na Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam imemwamuru Selasini kumlipa Mbatia kiasi cha shilingi milioni 80 kama fidia ya kumchafua, kulipa gharama za shauri pamoja na kumwomba radhi.
Wakili wa Mbatia, Hudson Mchau amesema hukumu hiyo imetolewa Mei 02, 2024 chini ya Hakimu Aron Lyamuya kufuatia maneno ya kashfa na udhalilishaji aliyoyasema Selasini dhidi ya Mbatia akiwa katika mkutano mjini Musoma mkoani Mara.
”Mahakama iliamuru kwamba maneno alioyaongea ndugu Joseph Selasini huko Musoma yalikuwa ni maneno ya udhalilishaji hivyo iliamuru aweze kuomba radhi ‘either’ [ama] kwa kwenda Musoma alipoweza kutoa maneno yale au aweze kutoa katika gazeti ambalo linasambazwa na eneo kubwa la nchi katika ukurasa wa mbele,” amesema.
Aidha, akizungumzia uamuzi huo wa mahakama Mbatia ameeleza kuwa “jaribio ovu la kutweza utu wangu limeshindwa, mahakama imeongea, asante sana mahakama.”