Mahakama yabadili utaratibu uendeshaji kesi ya Mbowe

0
36



Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam imeahirisha kesi inayomkabili Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe na wenzake hadi Agosti 6, 2021.

Akizungumza na waandishi wa habari, wakili wa Mbowe, Peter Kibatala amesema mahakama imeahirisha kesi hiyo iliyokuwa inafanyika kwa njia ya ‘video conference’ kutokana na changamoto za mtandao, na hivyo imeamuru watuhumiwa hao wapelekwa mahakamani kesho.

Kesi hiyo ikiendelea Mbowe na wenzake walikuwa katika Gereza la Ukonga, Dar es Salaam.

“Teknolojia imefeli hivyo tumeshindwa kufanikisha mchakato huo kwa sababu kumekuwa na mawasiliano hafifu kati ya video conference facility za hapa katika Mahakama ya Kisutu na Gereza la Ukonga na tumekubaliana kwamba kesho washitakiwa waletwe mahakamani,” amesema Kibatala.

Wakati kesi hiyo ikiendelea jeshi la polisi limewakamata baadhi ya wafuasi/wanachama wa CHADEMA waliofika katika mahakama hapo baada ya kuinua mabango huku wakisema “Mbowe sio gaidi.”

Katika kesi ya msingi Mbowe anakabiliwa na mashitaka mawili, la kwanza likiwa ni kula njama kulipua vituo vya mafuta na mikusanyiko ya watu vitendo vinavyohatarisha usalama wa raia na kuwatia hofu raia wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Anatuhumiwa kutenda kosa hilo katika tarehe tofauti kati ya Mei 1, 2020 na Agosti 1, 2020 katika Hoteli ya Aishi iliyopo wilayani Moshi mkoani Kilimanjaro.

Shitaka la pili, anatuhumiwa kufadhili uhalifu ambapo katika tarehe, eneo tajwa na maeneo mengine ya Dar es Salaam, Morogoro na Arusha alitoa fedha kwa watu huku akiamini zingetumika katika vitendo vya kigaidi vya kulipua vituo vya mafuta, mikusanyiko ya watu, vitendo vinavyotishia usalama na kutisha raia wa Tanzania.

Mbowe alifikishwa mahakama mara ya kwanza Julai 26 mwak huu baada ya kukamatwa mkoani Mwanza alipokuwa kwa ajili ya kushiriki kongamano la katiba mpya.

Send this to a friend