Mahakama yabatilisha Tigo kuwalipa Mwana FA na AY bilioni 2

0
45

Mahakama Kuu, Dar es Salaam, imebatilisha uamuzi uliotolewa kwa kampuni ya mawasiliano ya simu za mkononi MIC Tanzania Limited (Tigo) kuwalipa wanamuziki Hamisi Mwinjuma (Mwana-FA) na Ambwene Yesaya (AY) TZS bilioni 2.18 kwa kukiuka sheria za hatimiliki.

Mahakama hiyo imetoa uamuzi huo kufuatia rufaa ya Tigo iliyojikita kuonesha kuwa Mahakama ya Wilaya ya Ilala iliyotoa hukumu hiyo haikuwa na uwezo wa kusikiliza shitaka hilo.

Uamuzi huo uliotolewa na Jaji Joacquine De-Mello umekuja wakati wanamuziki hao waliofungua kesi hiyo mwaka 2012 wakiishitaki Tigo kwa kutumia nyimbo zao kama muito wa simu bila kibali wakiwa tayari wameshalipwa fedha hizo.

Tigo kupitia kwa wakili wake Rosan Mwambo imesema kuwa itawaandikia barua wasanii hao warejeshe fedha hizo, na endapo hawatafanya hivyo, (Tigo) itaomba kibali cha mahakama kukamata mali zao.

Katika kesi ya msingi namba 17 ya mwaka 2012, wasanii hao waliiomba Mahakama ya Wilaya ya Ilala itamke kuwa MIC iliingilia haki zao kwa kutumia kibiashara kazi zao za kimuziki walizozitunga kwa pamoja na kuzisajili katika Chama cha Hakimiliki na Hakishiriki Tanzania (COSOTA), Septemba 24,2010.

Aidha, waliiomba kulipwa fidia ya TZS bilioni 4.3.

Hukumu ya kesi hiyo ilitolewa Aprili 11, 2016 ambapo mahakama iliridhika kuwa Tigo ilikiuka Sheria ya Hakimiliki na Hakishiriki kwa kutumia kibiashara nyimbo zao ambazo ni Usije Mjini na Dakika Moja kama miito ya simu bila ridhaa wala makubaliano nao.

Tigo haikuridhika na uamuzi huo na ilikata rufaa Mahakama Kuu kupinga hukumu hiyo.

Send this to a friend