Mahakama Kuu ya Kanda ya Dar es Salaam imebatilisha uamuzi wa Baraza Kuu la Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) la kuwavua uanachama wabunge wa Viti Maalum, Halima Mdee na wenzake 18 ambao walituhumiwa kwenda Dodoma kuapishwa bila idhini ya chama.
Akitoa uamuzi leo Desemba 14, 2023 Jaji Cyprian Mkeha amesema kitendo cha wajumbe wa Kamati Kuu kuwa pia wajumbe wa Baraza Kuu na kutoa uamuzi wa rufaa ni kinyume cha kanuni za haki asili.
Wakili wa wabunge hao, Edson Kilatu ameishukuru mahakama kwa kutenda haki huku akisema “yapo baadhi ya maeneo ambayo pengine tulistahili kupata zaidi lakini tumepata pungufu ya kiwango kwa mfano mahakama kusema imebatilisha maamuzi ya baraza kuu lakini imeachia maamuzi ya kamati kuu.
Kwa maana kwamba CHADEMA itatakiwa iende ikazingatie sheria pamoja na taratibu za chama kwenda kuwasikiliza kwenye ngazi ya baraza kuu peke yake. Lakini sisi tunaona ilitakiwa maamuzi kuanzia ya kamati kuu yalitakiwa yaweze kubatillishwa,” amesema.
Kwa upande wa CHADEMA, wakili wa chama hicho, Dickson Matata amesema mahakama imefuta maamuzi ya rufaa ya baraza kuu lakini uamuzi ya kuwafuta uanachama ambayo yalitolewa na kamati kuu ya chama yako pale pale, huku chama hicho kikieleza kuwa kitaitisha upya baraza kuu na kufuata sheria kuwavua uanachama.
Mzozo kati ya CHADEMA na wabunge hao ulianza mara baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2020, ambapo chama hicho kilipinga matokeo na kugoma kupeleka majina ya wabunge wa viti maaalumu kwa kile ilichoeleza kutoridhishwa na mchakato mzima wa uchaguzi.
Hata hivyo, wabunge hao waliapishwa na aliyekuwa Spika wa Bunge, Job Ndugai kama wabunge wa viti maaalumu wa CHADEMA, lakini chama kilikana kuwatambua kikisema hakikuwasilisha jina lolote la wabunge hao na kamati kuu kuamua kuwafukuza uanachama ndipo wabunge hao walikata rufaa baraza kuu.
Baraza hilo liliunga mkono uamuzi ya kamati kuu ya chama hicho ya kuwafukuza uanachama kabla ya wabunge hao kwenda mahakamani, ambapo mahakama ilitupilia mbali maombi yao.