Mahakama yaelekeza Jeshi la Polisi kuwasaka walipo kina Soka na wenzake
Mahakama Kuu Dar es Salaam, imelielekeza Jeshi la Polisi kufanya upelelezi kujua mahali walipo viongozi wa Baraza la Vijana CHADEMA (BAVICHA) Wilaya ya Temeke wanaodaiwa kupotea tangu Agosti 18, mwaka huu.
Akitoa taarifa hiyo, Wakili Peter Madeleka ambaye anasimamia upande wa mashtaka dhidi ya Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IGP) Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es saalam, Mkuu wa Upelelezi Wilaya ya Temeke, Mkurugenzi wa Mashtaka na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, amesema mahakama imesema hakuna ushahidi unaoonesha kwamba viongozi hao wa BAVICHA wanashikiliwa na Jeshi la Polisi kinyume cha Sheria.
Aidha, Wakili Madeleka amesema upande wa mashtaka haujaridhishwa na uamuzi huo uliotolewa na mahakama, hivyo watakata rufaa ili kuhakikisha watu hao wanapatikana na watekaji wanawajibishwa kwakuwa wana ushahidi.
Viongozi hao waliopotea ni Mwenyekiti wa Wilaya ya Temeke, Deusdedith Soka na Katibu wake, Jacob Mlay pamoja dereva wao wa pikipiki, Frank Mbise, ambao wamedaiwa kupigiwa simu polisi kwenda kufuatilia suala la pikipiki ya Soka iliyodaiwa kuibiwa.