Mahakama yakataa ombi la mawakili wa Sabaya

0
45

Mahakama ya hakimu mkazi Arusha, imetupilia mbali pingamizi lililowasilishwa na mawakili wa utetezi katika kesi ya uhujumu uchumi inayomkabili aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai, Lengai Ole Sabaya na wenzake sita.

Hakimu mkazi wa Mahakama hiyo, Patricia Kisinda ametoa uamuzi huo mdogo wakati shahidi wa 3 wa Jamhuri, Adnabest Marandu ambaye ni mlinzi katika garage inayomilikiwa na Francis Mrosso, akiendelea kutoa ushahidi wake.

Wakati shahidi huyo akitoa ushahidi wake Mahakamani hapo akiongozwa na wakili wa serikali mwandamizi, Tarsila Gervas , mawakili wa utetezi waliwasilisha pingamizi wakipinga daftari la kumbukumbu ya magari yanayoingia na kutoka katika garage hiyo lisipokelewe kama kielelezo.

Hakimu Kisinda ambaye aliahirisha kesi hiyo kwa muda wa zaidi ya saa moja, akitoa uamuzi huo mdogo, amesema mahakama imetupilia mbali pingamizi hilo kwa kuangalia ushahidi uliotolewa na shahidi huyo wa 3 ambaye ameeleza mahakama kuwa ana uelewa na kielelezo hicho ambacho anaomba kipokelewe mahakamani hapo kama kielelezo na kuwa kimefuata matakwa ya kisheria.

Awali mawakili wa utetezi Mosses Mahuna, Fridolin Gwemelo na Edmund Ngemela waliwasilisha pingamizi hilo wakidai kielelezo hicho kimetolewa kwenye mikoba ya wakili Tarsila na kuwa hawaelewi amekipata wapi na kumtaka shahidi akitoe mahakamani hapo.

Wakili Mahuna amedai mahakamani hapo kuwa kielelezo hicho kikipokelewa mahakamani wakati hakijatoka kwa shahidi mwenyewe ushahidi huo utakuwa haujapatikana kwa kufuata sheria hivyo kuomba mahakama ikatae kupokea kielelezo hicho.

Mawakili wa serikali waliomba mahakama kutupilia mbali pingamizi hilo na mahakama ipokee kwani kimefuata taratibu za kisheria ikiwemo shahidi anayeomba kipokelewe kuwa anakijua kielelezo hicho na amekua akikiandaa.

Send this to a friend