
Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkuu Entebbe nchini Uganda imemkuta na hatia mtumiaji wa Tiktok, Juma Musuuza, maarufu Madubarah, kwa makosa sita, yakiwemo kutoa maneno ya chuki na kusambaza taarifa za uongo dhidi ya Rais Yoweri Museveni, mwanae, Jenerali Muhoozi Kainerugaba, na Spika wa Bunge Anita Among.
Madubarah ambaye pia ni mfanyabiashara wa viatu alidaiwa kutumia akaunti yake ya TikTok kuposti video mwaka 2024 akimkejeli Rais Museveni na mwanawe, akisema “Ikiwa Museveni atakabidhi madaraka kwa mwanawe mlevi, nchi itaangamizwa ndani ya siku mbili.” Pia alimtuhumu Spika Among kwa kutumia vibaya fedha za walipa kodi kujenga jumba la kifahari kuliko Ikulu na kununua vipodozi vya kujichubua.
Ushahidi wa upande wa mashtaka uliwasilishwa na mashahidi watatu, akiwemo maafisa wa polisi na Jeshi la Ulinzi Maalum (SFC). Hakimu Edgar Tibayeita Tusiime amesema ushahidi huo ulithibitisha nia ya Musuuza kudhalilisha viongozi.
Mwendesha mashtaka wa serikali, Paul Ahebwa, amesema kesi ya Musuuza ni sehemu ya ongezeko la watu kutumia mitandao ya kijamii kuchochea chuki wakijificha nyuma ya uhuru wa kujieleza.
Upande wa utetezi, wakili mkuu Jonathan Elotu aliomba adhabu nyepesi, akisema Musuuza ndiye anayeisaidia familia yake, na kwamba ni kosa lake la kwanza na tayari amekaa rumande zaidi ya miezi 10. Wakili mwingine wa utetezi, Mahad Kawuma, aliongeza kuwa kumpa kifungo kikali kutamnyima tu haki ya kikatiba ya uhuru wa kujieleza na kuwatisha wananchi wengine.







