Mahakama ya Hakimu Mkazi Kinondoni mkoani Dar es Salaam imetoa siku 21 kwa aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda kuwasilisha hati kinzani dhidi ya maombi yaliyofunguliwa na aliyekuwa Mbunge wa Ubungo, Saed Kubenea, kutaka kibali cha kumfungulia kesi ya jinai.
Mahakama imetoa maelekezo hayo baada ya Wakili wa Makonda, Goodchance Reginald kuwasilisha maombi ya kuongezewa muda wa kujibu hoja za mawakili wa Kubenea kwa madai kuwa mteja wake hakupata hati ya wito wa mahakama.
Mahakama yaruhusu Makonda kushitakiwa kwa makosa ya jinai
Wakili wa Kubenea, Hekima Mwasipu amepinga hoja za wakili huyo na kuhoji kwamba kama mteja wake hana taarifa imekuwaje yeye (wakili wake) yupo mahakamani kwenye shauri hilo?
Hata hivyo wakili Reginald amesema mteja wake alipata taarifa kupitia vyombo vya habari, hivyo akaona afike mahakamani licha ya kuwa hakukuwa na taarifa rasmi za mahakama.
Paul Makonda aongezewa mashitaka
Isome hapa hati ya mashitaka yanayomkabili Paul Makonda
Awali Wakili wa Serikali Mwandamizi, Subira Mwalumuli, ameeleza mahakama hiyo kuwa Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai DCI na Mkurugenzi wa Mashtaka nchini DPP wanakusidia kupeleka mapingamizi ya awali dhidi ya maombi yaliyowasilishwa kwenye kesi hiyo kwa madai kuwa ufunguaji kesi hiyo una mapungufu ya kisheria.
Kesi hiyo imeahirishwa hadi Machi 25 mwaka huu, ambapo wajibu maombi watatakiwa kuwasilisha hati kinzani huku upande wa Jamhuri (DCI na DPP) wakiwatakiwa kuwasilisha hoja za mapingamizi yao juu ya shauri hilo.