Mahakama yamtambua Doreen kama mnufaika wa mali za Mrema

0
41

Sakata la nani anastahili kunufaika na mali za aliyekuwa mwanasiasa mashuhuri nchini, Augustino Mrema limetolewa majibu baada ya mahakama Kuu ya Tanzania, Masijala Ndogo ya Temeke mkoani Dar es Salaam kumtambua mjane wa marehemu, Doris Mkandala maarufu Doreen kuwa mmoja wa wanufaika wa mali hizo.

Katika hukumu iliyotolewa na Jaji Augustine Rwizile Oktoba 24, mwaka huu imewajumuisha pia watoto watatu wa Mrema waliozaliwa nje ya ndoa kama wanufaika wa mali za mwanasiasa huyo, sambamba na watoto wa marehemu ambao walizaliwa ndani ya ndoa.

Watoto hao wa nje ya ndoa ni Elizabeth Mrema (52), Elizabeth Mrema (43) na Goodlove Mrema (18), wakiungana na watoto wengine wa Mrema, Mary Mrema (48), Cresensia Mrema (45), Michael Mrema (40), Edward Mrema (38) na Peter Mrema (37).

Ndoa ya Doreen na Mrema ilifungwa Machi 24, 2022 katika Parokia ya Uwomboni, Jimbo Katoliki la Moshi, wakati huo Mrema akiwa na umri wa miaka 77 na Doreen akiwa na umri wa miaka 38.

Baada ya kifo cha Mrema Agosti 21, 2022, kuliibuka mvutano kati ya makundi mawili; kundi moja likiwa ni mke wa marehemu na watoto waliozaliwa nje ya ndoa, na Peter Mrema (37) aliyeteuliwa na kikao cha familia kuwa msimamizi wa mali ambaye alikuwa kwenye kundi la watoto wa marehemu akipinga Doreen kuwa msimamizi mwenza wa mali kwa madai kuwa siyo mtu wa kuaminika.

Send this to a friend