Mahakama yatangaza nafasi za ajira mpya 207

0
11

Tume ya Mahakama kupitia Ofisi ya Menejimenti ya Utumishi wa Umma imetangaza nafasi mpya za ajira 207 za sekta ya mahakama katika kada tisa tofauti.

Akitangaza nafasi hizo Katibu wa Tume, Elisante Ole Gabriel kupitia vyombo vya habari jijini Dar es salaam, amezitaja nafasi hizo kuwa ni mahakimu 20, ofisa hesabu daraja la pili nafasi sita, msaidizi wa hesabu nafasi 11, maofisa utumishi nafasi nne, na nafasi tano za maofisa rasilimali watu na utawala.

Aidha nafasi zingine ni 35 za madereva daraja la pili, nafasi 80 za makatibu muhtasi, nafasi 38 za wasaidizi wa kumbukumbu na nafasi nne za maofisa ukaguzi wa ndani.

Elisante ameongeza kuwa nafasi hizo haziwahusu wafanyakazi wa Serikali na taasisi zake, badala yake ni kwa ajili ya watumishi walio katika sekta binafsi na wale ambao hawana ajira kabisa.

Ameendelea kusisitiza kwa waombaji kuzingatia mambo muhimu yaliyoorodheshwa hasa katika kipengele cha 12 katika tangazo hilo kabla ya kuanza kuomba ili kuepuka usumbufu.

Amewasihi waombaji kuepuka matapeli kwani tangazo halali linapatikana kwenye tovuti ya tume ya www.jic.go.tz.

Send this to a friend