
Mwenyekiti wa CHADEMA, Tundu Lissu ameieleza mahakama kuwa hayuko tayari shauri lake kuendelea kusikilizwa mpaka pale majaji watakapotoa uamuzi juu ya mambo yanayoendelea nje ya mahakama ikiwemo wanachama kuzuiwa kuingia mahakamani.
Hayo yamesemwa na Kaimu Katibu Mkuu wa CHADEMA, John Mnyika mara baada ya viongozi wa chama hicho kususia kusikiliza kesi hiyo na kutoka nje ya mahakama kama ishara ya kupinga Askari Polisi kuzuia wananchi kuingia mahakamani.
“Taarifa ambayo nimepewa na washauri wa Lissu ni kwamba, Mheshimiwa Lissu amewaeleza majaji juu ya haya ambayo yanayoendelea kutendeka nje ya chumba cha mahakama, na ameweka msimamo wake kwamba hayuko tayari shauri kuendelea kusikilizwa mpaka kwanza apewe nafasi ya kuwaeleza majaji kuhusu jambo hili na majaji waweze kulitolea uamuzi,” amesema.
Hata hivyo, Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala ndogo ya Dar es Salaam imetupilia mbali hoja ya Lissu aliyodai kuwa Polisi kupitia amri ya ZCO waliwatoa viongozi na wanachama wa CHADEMA waliofika Mahakamani hapo kusikiliza mwenendo wa kesi, ikieleza kuwa hakuna amri yoyote iliyotolewa Mahakamani hapo.







