
Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala Kuu Dodoma imetupilia mbali kesi ya kikatiba iliyofunguliwa na mwanachama wa ACT-Wazalendo, Luhaga Mpina pamoja na ACT- Wazalendo kupinga kuondolewa kwenye orodha ya wagombea Urais wa Tanzania.
Mahakama imeeleza kuwa haina mamlaka ya kuingilia uamuzi wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) unaotekelezwa kwa mujibu wa Katiba na sheria.
Shauri hilo limesikilizwa mbele ya jopo la Majaji watatu wakiongozwa na Jaji Frederick Mayanda, huku upande wa waleta maombi ukiongozwa na Wakili John Seka na timu yake ya mawakili. Wadaiwa katika shauri hilo walikuwa ni Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) pamoja na Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
Aidha, Wakili wa waleta maombi, John Seka, ameiambia Jambo TV kuwa rufaa ipo wazi kwa wateja wake endapo wataamua kupinga uamuzi huo.






