Mahakama yawatoza faini ya laki 3 waliomteka mwanamke kwa siku nne

0
41

Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam imewahukumu wanaume sita kulipa faini ya shilingi 300,000 au kwenda jela miaka mitatu kila mmoja, baada ya kupatikana na hatia ya kumteka na kumshikilia mwanamke kwa siku nne mfululizo.

Washtakiwa hao, Assad Abdulrasur (43) mkazi wa Msasani Village, Fahad Mussa (32) mkazi wa Dodoma Airport, Nathan Jothan (27) mkazi wa Sinza, Nicolas Nilahi (39) mkazi wa Wazo Hill, Fredy Chahoza (49) mkazi wa Chamwino Dodoma na Ifan Saleh (41) mkazi wa Kisemvule, Dar es Salaam walimteka Han Nooh Hussein eneo la Msasani Beach, wilaya ya Kinondoni, Dar es Salaam Oktoba 16, 2023.

Uamuzi huo umetolewa Machi 6, 2024 na Hakimu Mkazi Mkuu, Aaron Lyamuya, baada ya washtakiwa hao kufanya majadiliano na Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) ya kuimaliza kesi.

Aidha, mahakama hiyo imeamuru kila mshtakiwa kumlipa mlalamikaji fidia ya shilingi 500,000 kwa kumsababishia maumivu na mateso kutokana na kumshikilia kwa siku nne mfululizo katika nyumba ya Haidary Waziri iliyopo eneo la Msasani Beach.

Send this to a friend