
Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam imekubali ombi la Jamhuri la kuzuia urushaji, utangazaji na usambazaji wa moja kwa moja (mubashara) wa mwenendo wa mashahidi katika kesi ya uhaini inayomkabili mwenyekiti wa CHADEMA, Tundu Lissu, hadi itakapoamuliwa vinginevyo.
Jamhuri iliwasilisha ombi hilo ili kulinda utambulisho wa mashahidi kwa lengo la kutohatarisha usalama wao.
Hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama hiyo, Franco Kiswaga amesema mtu au chombo cha habari kitakachokiuka amri hiyo, hatua stahiki zitachukuliwa kwakuwa ilikuwa ni amri halali ya Mahakama Kuu.
“Kila mtu au kituo cha Habari au wanahabari kinachotaka kuchapisha mwenendo wa mashahidi ni lazima kilete ombi mahakamani rasmi,” amesema Hakimu Kiswaga.
Aidha, mahakama imewataka Jamhuri kuhakikisha kabla nyaraka za ushahidi kusomwa mahakamani, zizingatie maagizo ya Mahakama Kuu kwa kuchakata na kuhariri taarifa za mashahidi zinazoweza kusababisha mashahidi kutambulika.







