Serikali imesema mpango wa kurudisha vyura wa Kihansi ulianza tangu mwaka 2012 na kufikia Juni mwaka huu, vyura wote waliobaki watakuwa wamerudishwa kutoka Marekani.
Mkurugenzi Mwendeshaji wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), Maharage Chande amesema vyura hao walipaswa kurejeshwa nchini mwaka 2019, lakini sababu ya mlipuko wa UVIKO – 19 mpango huo ulishindikana, hivyo Serikali ikaongeza mkataba wa miaka miwili kuwahifadhi, na mpaka sasa jumla ya vyura 12000 wamerudishwa.
Ameongeza kuwa Serikali inakusudia kuwahifadhi vyura hao katika Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA), Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) na mahali pao pa asili, Kihansi.
Bibi wa miaka 78 akamatwa kwa kupora pesa benki
Maharage amesema katika mpango wa kimaendeleo, Serikali iliamua kuwa na mipango yote miwili, kuwalinda vyura na kisha kuzalisha umeme.
“Ikiwa hatuna mpango wa kuwalinda, tusingeweza kuwa na mradi wa kuzalisha nishati hiyo pale Kihansi,” amesema.
Vyura hao ambao hawapatikani mahali pengine popote isipokuwa katika bonde la Kihansi nchini Tanzania, waligunduliwa mwaka 1996 na kupelekwa nchini Marekani mwaka 2000.