Majaji na Mahakimu wanawake wampongeza Rais kuteua wanawake

0
44

Rais Samia Suluhu Hassan amekutana na kufanya mazungumzo na uongozi wa Chama cha Majaji na Mahakimu Wanawake Tanzania (TAWJA), Ikulu Chamwino mkoani Dodoma.

Katika mazungumzo hayo, Mwenyekiti wa TAWJA, Jaji Joaquine De-Mello amempongeza Rais Samia kwa kushika nafasi ya uongozi na kuwa Rais wa kwanza Mwanamke nchini Tanzania.

Jaji De-Mello amesema Chama cha Majaji na Mahakimu wanawake Tanzania (TAWJA), kinafarijika na uongozi wake kutokana na mambo mbalimbali anayofanya ikiwa ni pamoja na kuzingatia usawa wa kijinsia kwa kuongeza idadi ya wanawake katika nafasi mbalimbali za uongozi.

Amesema TAWJA iko tayari kushirikiana na Serikali katika kusimamia haki pamoja na kuhakikisha Serikali inafikia lengo la usawa wa kijinsia wa 50 kwa 50 katika ngazi mbalimbali za uongozi.

Kwa upande wake Rais Samia amekishukuru Chama cha Majaji na Mahakimu wanawake Tanzania (TAWJA) kwa kazi nzuri inayofanya na kuahidi kuendelea kushirikiana nao katika kutekeleza majukumu yao na amepokea changamoto zao na kuahidi kuzifanyia kazi.

Send this to a friend